Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali ya Awamu ya Sita Yafanya Marekebisho Makubwa Sekta za Habari, Mawasiliano
Mar 14, 2022
Na Jacquiline Mrisho

. Na Grace Semfuko, MAELEZO

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Madarakani, Wizara yake imeanza mapitio ya Sera tatu kati ya nne zinazoongoza Wizara yake kwenye sekta mbalimbali ili kuziboresha na hatimaye ziweze kuendana na wakati tulio nao sasa.

Amezitaja sera hizo kuwa ni pamoja na Sera ya Taifa ya Mawasiliano ya Simu ya Mwaka 1997, Sera ya Taifa ya Posta na Sera ya Habari na Utangazaji zote zikiwa ni za mwaka 2003.

Akizungumzia mafanikio ya mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani, Waziri Nape amesema yapo mambo mengi yamefanyika katika kipindi hicho ikiwepo pia mapitio ya sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayoendesha wizara hiyo, lengo likiwa ni kuzipa nguvu na uwezo wa kukidhi mahitaji ya uendeshaji wake.

“Katika kipindi cha mwaka mmoja wakati Rais Samia anaingia madarakani aliagiza sera hizi zipitiwe upya, aliagiza tupitie sera, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali zinazoendesha sekta hizi za Wizara yetu, ili kuoingeza wigo, kuziboresha na kuzipa uwezo wa kufanya kazi, sasa Sera mbalimbali zinazopitiwa ni za muda mrefu ukiacha Sera ya TEHAMA ya mwaka 2016, lakini sera zingine zote tunazipitia ili tuone namna ya kuziboresha ili zikidhi mahitaji kwa wakati na mazingira tuliyo nayo”, amesema Waziri Nape.

Nape pia amesema kuwa Wizara hiyo imeandaa mapendekezo ya kutungwa kwa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi, kwa lengo la kusaidia kuingia katika uchumi wa kidigitali ambapo kukamilika kwa sheria hii kutakuwa ni kichocheo cha uwekezaji katika biashara mbalimbali zinazotumia mitandao na mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji, uchakataji na ubadilishanaji wa taarifa binafsi nchini.

“Sheria hii iko kwenye hatua za mwisho kabisa, tumeshafanya mchakato ndani ya mwaka mmoja hii sheria ni muhimu kwa sababu vinginevyo uwekezaji utakuwa mgumu na kelele imekuwepo ya muda mrefu na ni kelele ya kidunia nzima kuwepo na ulinzi na kutunza siri za watu lakini pia dunia ndipo ilipo, ukitaka watu wawekeze kwenye data lazima wawe na hakika kwamba wako salama”, amesema Waziri Nape.

Aidha, Waziri Nape pia amebainisha kuwa kanuni za maudhui ya mtandao za mwaka 2020 pia zimefanyiwa marekebisho ambapo sasa zimeondolewa leseni kwa watoa maudhui mbalimbali yakiwepo ya mapishi, michezo, usanii, filamu, muziki na mengineyo mengi na leseni hizo zikiachwa kwa vyombo vya habari vya kawaida na kwa wakusanya habari mbalimbali wenye lengo la kuzitoa kwa watoa maudhui ya habari mitandaoni.

Ameyataja mambo mengine yaliyorekebishwa kuwa ni kuondoa zuio la matangazo ya michezo ya kubahatisha, kupunguza ada ya mwaka ya leseni ya maudhui ya mitandaoni kutoka shilingi milioni moja hadi kufikia shilingi laki tano.

Katika hatua nyingine Waziri Nape amesema kutokana na marekebisho ya sheria na kanuni mbalimbali, kumekuwa na ongezeko la uwekezaji katika vyombo vya habari nchini katika kipindi hicho cha mwaka mmoja ambapo redio zimeongezeka kutoka 119 hadi kufikia 210 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 76.6% televisheni kutoka kutoka 44 hadi kufikia 56 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 27.3% cable televisheni kutoka 37 za mwezi februari 2021 hadi kufikia 59 februari 2022 ikiwa ni sawa na ongezejko la asilimia 59.5% na magazeti kutoka 270 hadi kufikia 284 ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.2%

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi