Na Magdalena Nkulu, Shinyanga
Serikali Mkoani Shinyanga imefunga rasmi shughuli za uchenjuaji dhahabu katika eneo la Bushushu kata ya Ngokolo, manispaa ya Shinyanga baada ya kujengwa katikati ya makazi ya watu hivyo kuleta athari kwa wananchi kutokana na sumu kali inayotumika kwa kazi hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Ally N. Rufunga amefunga shughuli hizo mapema leo baada ya kutembelea eneo hilo na kujiridhisha kuwa hapastahili kufanya kazi za aina hiyo na amesema amefanya hivyo ili iwe fundisho kwa wengine.
Mhe. Rufunga amesema kuwa, uamuzi huo unafuatia malalamiko ya baadhi ya wananchi wa eneo hilo kuwa kuna viwanda vinavyojihusisha na uchenjuaji wa dhahabu ambapo Halmashauri ya Manispaa ilishawasimamisha wamiliki wake kuendelea na shughuli hizo lakini walikaidi, hivyo aliamua kufanya ziara akiambatana na Mhe. Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Bi Anna Rose Nyamubi pamoja na wataalamu wa manispaa ya Shinyanga.
Akiwahoji wamiliki hao ambao ni Bw.Kija Makindo wa Nyoda Investment pamoja na Bw.Ezekiel Allen William (Mbwambo) kwa nyakati tofauti alipotembelea kwenye viwanda hivyo, walikiri kuwa, awali walinunua viwanja hivyo kwa ajili ya kujenga makazi lakini walibadili matumizi na kufanya viwanda vya kuchenjua dhahabu.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ameagiza Bw. Mbwambo kupelekwa mahakamani kwa kosa la kuendesha mradi huo bila leseni ya Ofisi ya Madini Mkoa ambao walimsimamisha tangu mwezi Novemba mwaka jana ili wakamilishe taratibu za kutoa leseni lakini alikaidi amri hiyo na kuendelea kuzalisha.
Ofisi ya Mazingira Manispaa pia imedai iliwashauri wamiliki hao kufuata taratibu zote za tathmini ya athari za mazingira kwa kuwasiliana na Baraza la Mazingira la Taifa yaani (NEMC) ili wapate vyeti lakini wameshindwa kufanya hivyo.
Hata hivyo, mmiliki mmoja Bw. Makindo ameomba kupewa muda zaidi ili akamilishe taratibu za kuhamisha vifaa kabla ya kufunga kiwanda chake ambapo amepewa siku 30.