Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali, Sekta Binafsi Kukuza Diplomasia ya Uchumi
Apr 06, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Jonas Kamaleki

Serikali imesema itashirikiana na sekta binafsi ili kukuza na kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa ajili ya maendelo endevu ya wananchi.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhani Mwinyi wakati akipokea michango ya wadau kwa ajili ya maandalizi ya maonesho ya bidhaa za viwanda vya Tanzania yatakayofanyika nchini Kenya mwezi huu (Aprili, 2018).

"Diplomasia za mahusiano na kisiasa kwa sasa hazina nafasi, mkazo ni kwenye diplomasia ya kiuchumi kwa ajili ya maendeleo"alisema Balozi Mwinyi.

Waliotoa michango yao kwa ajili ya tukio hili ni pamoja na Lake Oil, Bravo Logistics, IPP Media, KNAUF Gypsum Tanzania Ltd na Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN).

Naibu Katibu Mkuu amendelea kusema kuwa wakati wa kuuza malighafi na kununua bidhaa kwa sasa ufikie mwisho ili Tanzania itengeneze bidhaa na kuziuza kwenye soko la Afrika Mashariki ambalo lina watu zaidi ya milioni 300.

Amesema kuwa hii ni fursa ambayo watanzania hawana budi kuitumia kwani uwezo wa kuchakata mazao na kutengeneza bidhaa na kuziuza nje upo.

Balozi Mwinyi ameipongeza sekta binafsi kwa kushirikiana na Serikali katika kukuza diplomasia ya uchumi hususan katika kuunga mkono jitihada za Serikali kupeleka bidhaa za Tanzania nje ya mipaka ya nchi.

Aidha, Balozi Mwinyi alisema kuwa msukumo huo wa diplomasia ya uchumi unatokana na kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuifanya nchi kuwa na uchumi wa kati unaotokana na viwanda.

Amesema kuwa Tanzania imekuwa ikipokea bidhaa nyingi toka Kenya na kuongeza kuwa sasa wakati umefika wa Watanzania kuingia katika soko la Kenya.

"Inabidi twende Kenya kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa kishindo kwani taarifa nilizo nazo ni kwamba wazo hilo limepokelewa vizuri nchini humo", aliongeza Balozi Mwinyi.

Hivyo amewaomba wafanyabiashara wajitokeze kwa wingi kupeleka bidhaa zao nchini Kenya pia wachangie katika shughuli hii nzima.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Edwin Rutageruka amesema kuwa hii ni fursa nzuri kwa wafanyabiashara nchini Tanzania kuingia katika soko la Kenya.

Rutageruka amesema kuwa wafanyabiashara wajitokeze kushiriki tukio hilo la kihistoria ili waweze kupanua wigo wa soko la bidhaa zao.

Ameishukuru Serikali kwa kutilia mkazo wa diplomasia ya uchumi ambayo itatoa matokeo makubwa kwa kuongeza kipato na ajira kwa watanzania.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Bravo Logististics, Angelina Ngalula ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Sekta Binafsi (TPSF) ameishukuru Serikali kwa kukuza diplomasia ya uchumi na kuongeza kuwa watanzania wajitahidi kuuza bidhaa za kitanzania katika nchi zilizoizunguka Tanzania, kwani ni soko la uhakika.

"Mchele wa Tanzania toka Kyela ni mzuri sana kuliko mchele karibu wa eneo lolote duniani, hivyo tukiuuza nje tuna uhakika wa kupata soko", amesema Ngalula.

Kuanzia mwezi Aprili 24 hadi Aprili 27 wafanyabiashara wa Kitanzania watashiriki maonesho na mazungumzo ya kibiashara jijini Nairobi, Kenya kwa ajili ya kuingiza bidhaa za Tanzania katika soko la Kenya.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi