Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali: Mfumuko wa Bei Nchini Washuka
Aug 09, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_8779" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi wa Idara ya Sensa na Takwimu Ofisi ya Taifa ya Takwimu Ephraim Kwesigabo akitoa ufafanuzi juu ya hali ya mfumuko wa bei kwa mwezi wa Julai 2017. Kwenye taarifa yake mfumuko wa bei nchini umepungua ukilinganisha na mfumuko wa bei kwa mwezi ulioishia Juni 2017. (Picha na Idara ya Habari Maelezo)[/caption]

Na: Bushiri Matenda

Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Julai, 2017 umepungua hadi kufikia asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 5.4 ilivyokuwa mwezi Juni, 2017. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa taarifa ya kila mwezi iliyotolewa leo jijini Dar-es-Salaam na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.

Mkurugenzi wa Idara ya Sensa na Takwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Ephraim Kwesigabo amesema kiwango hicho kipya cha mfumuko wa bei kwa Mwezi Julai inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2017 imepungua  ikilinganishwa na mwezi Juni, 2017.

Kupungua kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Julai, 2017 kumechangiwa hasa na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Julai, 2017 zikilinganishwa na bei za mwezi Julai, 2016.

Mkurugenzi huyo wa Sensa na Takwimu alieleza kuwa baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa Mfumuko wa Bei  ni pamoja na “nyama kwa asilimia 3.8, samaki wabichi kwa asilimia 14.1, dagaa kwa asilimia 8.4, kabichi kwa asilimia 16.6, biringanya kwa asilimia 10.6, vitunguu kwa asilimia 13.2, karoti kwa asilimia 16.9, njegere kwa asilimia 15.7 na viazi mviringo kwa asilimia 13“.

Vilevile alisisitiza thamani ya shilingi ya Tanzania imezidi kuimarika ambapo uwezo wa Shilingi 100 katika kununua bidhaa na huduma umefikia Shilingi 91 na senti 87 mwezi Julai, 2017 ikilinganishwa na Shilingi 91 na senti 66 ilivyokuwa mwezi Juni, 2017.

Akitoa mlingano wa mfumuko wa bei na nchi zingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki Mkurugenzi Kwesigabo alifafanua kuwa mfumuko wa bei nchini una mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki. Kwa mfano nchini Kenya Mfumuko wa Bei wa mwezi Julai, 2017 umepungua hadi asilimia 7.47 kutoka asilimia 9.21 mwezi Juni, 2017 na nchini Uganda umepungua hadi asilimia 5.70 mwezi Julai, 2017 kutoka asilimia 6.4 mwezi Juni, 2017.

Mfumuko wa Bei wa Taifa unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini kwa kipindi maalum.                                              

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi