Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea na uratibu wa uanzishaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika na tayari shilingi bilioni 15.7 zimekusanywa kutoka kwa wanahisa.
Amesema kiasi hicho ni sawa na asilimia 78.5 ya mtaji wa shilingi bilioni 20 zinazohitajika na kwamba kuanzishwa kwa benki hiyo, kutaviwezesha vyama vya ushirika kupata mikopo yenye riba nafuu na kuendesha shughuli zake kwa tija.
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 17, 2024) wakati akizungumza na wadau wa Kongamano la Kumi la Wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi lililofanyika katika ukumbi wa Jenerali Venance Mabeyo, jijini Dodoma.
"Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuchukua hatua mahsusi za kuimarisha ushirika hapa nchini. Hatua hizo ni pamoja na kufanya maboresho ya mifumo ya uendeshaji wa vyama vya ushirika ili kuongeza ufanisi."
Amesema Serikali imefanya maboresho ya kitaasisi kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi kwa kuunganisha Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania, Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania, Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania kuwa sehemu ya muundo wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).
Amesema serikali pia imeunganisha Bodi ya Chai Tanzania na Umoja wa Wakulima Wadogo wa Chai ili kuwa na Bodi moja. Pia imehamishia shughuli za Bodi ya Pareto Tanzania kwenda kwenye Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko.
"Kwa upande wa sekta ya mifugo na uvuvi, serikali inaendelea kukamilisha utaratibu wa kuunganisha Bodi ya Nyama na Bodi ya Maziwa, kuanzisha Mamlaka ya Usimamizi wa Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji pamoja na Mamlaka ya Bidhaa na Miundombinu ya Mifugo."
Amesema maboresho hayo ni sehemu ya jitihada za makusudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuongeza ufanisi na kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta hizo. Hivyo, ametoa wito kwa wadau wa kongamano hilo kujadili namna bora ya kuiwezesha Tanzania kuwa sehemu ya maendeleo ya kilimo smati.
Amesema hivi sasa dunia inaendelea kujadili suala la mabadiliko ya tabianchi, mifumo ya chakula, akilibandia, hewaukaa pamoja na masuala mazima ya ubunifu na teknolojia.
"Katika hizi siku tatu za Kongamano, hakikisheni mnajadili kuhusu masuala hayo na kuja na mapendekezo ya namna ya kuboresha sera zetu na mifumo yetu katika sekta hizi. Leteni mapendekezo ili twende na wakati, tuongeze tija, tukuze mitaji na uwekezaji kwenye sekta hizi muhimu katika uchumi wa nchi."
Mapema, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema katika kufanya maboresho ya sekta ya kilimo hususan sekta ya uzalishaji mbegu, Serikali imeanza utaratibu wa kuwawezesha wazalishaji binafsi wa mbegu kwa kuwatambua na kuwapatia mashamba ili kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za kilimo.
"Serikali inaendelea na mkakati wa kuona ni namna gani tunaweza kutoa ruzuku kwa wazalishaji wa mbegu ili nchi yetu iweze kujitosheleza katika uzalishaji wa mbegu bora.