Serikali kupitia Wizara ya Afya imedhamiria kuvilinda, kuvibeba na kuvilea viwanda vya ndani vinavyotengeneza bidhaa za dawa nchini hususan Maji Tiba (Drip) ili kuwaunga mkono na kuwavutia wawekezaji wengine.
Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu ameyasema hayo Oktoba 13, 2033 wakati alipotembelea katika kiwanda cha Alfa Pharmaceuticals kilichopo Mbagala Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.
“Nataka kuwahakikishia wazalishaji wa ndani wa dawa hususan Maji Tiba, Serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan itawalinda, itawalea na itawabeba, hatuwezi tukaacha uwekezaji huu mkubwa mlioufanya ukapotea, tutaendelea kununua Maji Tiba ndani ya nchi”. Amesema Waziri Ummy.
Katika kutekeleza hilo, Waziri Ummy amesema Serikali imeshaelekeza kwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na kufanya uamuzi wa kununua Maji Tiba katika viwanda vya ndani ili kuwaunga mkono wazalishaji wa ndani ya nchi kuanzia tarehe 1 Julai, 2023.
Aidha, Waziri Ummy ametoa rai kwa Watanzania hususan kwa wamiliki wa Hospitali, kuwaunga mkono wawekezaji wa ndani wanaozalisha bidhaa za dawa hususan Maji Tiba ili kuwavutia wawekezaji wengine kuja kuwekeza nchini.
Waziri Ummy amesema kuwa kiwanda hicho cha Alfa Pharmaceuticals kina uwezo wa kuzalisha chupa za Maji Tiba milioni 12 kwa mwaka na kiwanda cha Kairuki kinazalisha chupa milioni 37 kwa mwaka, hivyo viwanda viwili vinauwezo wa kuzalisha chupa milioni 49 kwa mwaka.
Akitoa faida za uwekezaji amesema, kuna faida nyingi za kuzalisha bidhaa za afya ndani ya nchi ikiwemo kuokoa fedha za Serikali, kupungua kwa gharama za bidhaa hizo pamoja na kupatikana kwa wakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha Alfa Pharmaceuticals, Bw. Bashir Haruni ameihakikishia Serikali kuwa itaendelea na uzalishaji wa bidhaa za dawa (Drip) kwa lengo la kuwahudumia Watanzania.
“Tutaendelea kuwekeza katika Sekta hii ya afya na tayari pia tumeshawekeza katika ujenzi wa Hospitali, naishukuru sana Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kuunga mkono jitihada hizi za kuwahudumia Watanzania”. Amesema Bw. Harun.