Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali kuufanya Uwekezaji Kiwanda cha Nyama SAAFI
Aug 18, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Serikali imedhamiria kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi katika mikoa yote nchini, ili kuimarisha uchumi, kupanua wigo wa walipa kodi, ajira na kuwawezesha wananchi kupunguza umasikini.

Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), kwa kushirikiana na Wizara ya mifugo na Uvuvi,  imedhamiria kuufanya uwekezaji wa kiwanda cha kusindika nyama cha SAAFI (Sumbawanga  Agricultural and Animal Food Industry), ili kiweze kuwa na uzalishaji mkubwa zaidi kulingana na uwezo wake wa mitambo na mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.

Akiongea mara baada ya kukamilisha ziara yake kiwandani hapo, mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Mhe. Geoffrey Mwambe, aliyeambatana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki. Mhe. Mwambe alifafanua kuwa Serikali itachambua kwa kina masuala ya uwekezaji wa kiwanda hicho kwa lengo la kuona namna ya kukiwezesha kiwanda hicho kiweze kuzalisha kwa ufanisi.

“Nimeambiwa kiwanda hiki kina masoko ndani ya Afrika kwa nchi za Comoro, Zambia na nje ya Afrika, huko Dubai. Kiwanda hiki kitaongeza faida kwa wanasumbawanga, kwa vijana kupata ajira, wafugaji kupata soko la mifugo yao pamoja na nchi itapata fedha za kigeni kwa kuuza nyama nje ya nchi”, alisistiza Mhe. Mwambe.

Mhe, Mwambe amebainisha kuwa uwekezaji katika Mkoa wa Rukwa ni muhimu kwa kuwa mkoa huo upo kwenye lango la soko la SADC, kwa kuwa karibu na Tunduma. Aidha, amefafanua kuwa kwa kulitambua hilo, serikali imeanza kuufungua mkoa huo kwa kutenga fedha katika bajeti ya fedha ya mwaka huu, za kujenga uwanja wa ndege mjini Sumbawanga.  

Amezitaka Mamlaka za Mikoa, Wilaya na Halmashauri kutenga maeneo ya uwekezaji pamoja na kuwa na miongozo ya fursa za uwekezaji. Aidha, amezishauri mamlaka hizo kuboresha maeneo hayo kwa kujenga miundo mbinu ili kuhamasisha na kuvutia wawekezaji. Pia, ameeeleza kuwa miongozo hiyo ni muhimu kwaniitaogeza kasi ya wawekezaji kuja Tanzania na kuwekeza kwenye maeneo ya vipaumbele vyao.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amefafanua kuwa kiwanda hicho kikiwezeshwa kuzalisha kwa ufanisi kitaweza kuwasaidia wafugaji wa mkoa huko kupata soko la uhakika la mifugo yao pamoja na kuweza kuongeza kipato.

Naye Mkurugenzi Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo ya SAAFI, Theresia Zumba Mzindakaya, ameishukuru serikali kwa nia yake ya kuendelea kuwasaidia ya kuhakikisha kiwanda hicho kinazalisha kwa kiwango cha malengo yao. Aidha, alimhakikishia Waheshimiwa Mawaziri kuwa ushauri na maelekezo waliyowapa watayatekeleza kwa wakati.

Kampuni ya SAAFI (Sumbawanga Agricultural and Animal Food Industries Limited) ni kampuni iliyosajiliwa mwaka 1989. Lengo kubwa la kuanzishwa kwa kampuni hiyo ilikuwa ni kuendeleza ranchi ya ngombe na kuanzisha kiwanda cha kusindika nyama. Kampuni hii inamilikiwa na familia ya Dkt. Chrisant Mzindakaya.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi