Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano imesema kuwa imeandaa utaratibu utakaowasaidia wahandisi wazawa kupata fursa ya kurithi teknolojia kutoka kwa wageni katika ujenzi wa miradi mikubwa ya nchi.
Akizungumza jana jijini Dar es salaam, wakati akifunga Kongamano la Maadhimisho ya miaka 50 ya Bodi ya Wahandisi sambamba na Siku ya Wahandisi nchini lililofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Elias Kwandikwa alisema kuwa hivi karibuni Bunge limepitisha sheria ya kumtambua mzawa katika shughuli za kihandisi hapa nchini.
“Kupitia wizara yangu kumekuwa na utaratibu wa kuangalia namna ya kuwasaidia wahandisi wazawa, kwa mfano miradi inayofikia gharama ya shilingi bilioni 20 lazima iachwe kwa wazawa peke yake, lakini kwa miradi mikubwa tunapoingia mkataba unatengenezwa kwa malipo yanayoweza kuwa kwa fedha za kigeni na malipo ya fedha za kitanzania , ambapo inatoa fursa kwa wageni kuwashirikisha wahandisi wa kitanzania katika kazi zao” alisema Naibu Waziri Kwandikwa
Aidha, aliongeza kuwa “katika sehemu ya ajira, Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB) nayo inasimamia katika kuhakikisha wahandisi wazawa wanahusishwa katika miradi iliyopo nchini ikiwa ni pamoja na kufanyakazi sambamba na wageni katika miradi wanayopata hapa nchini lengo likiwa ni kujenga uwezo na uzoefu mkubwa kwa wahandisi wazawa kuweza kufanyakazi, na hivi sasa matokeo yake yanaonekana ipo miradi mingi ambayo wahandisi washauri ni wazawa na wanafanyakazi kutokana kwa uzoefu walioupata kutoka kwa wageni”.
Hatahivyo, Naibu Waziri Kwandikwa alisisitiza wahandisi kuzingatia maadili na taratibu za kazi na wasiofanya hivyo watachukuliwa hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kunyang’anywa leseni za uhandisi, ili kuepuka maafa yanayoweza kusababishwa kutokana na uzembe katika kazi za kihandisi.
Katika Maadhimisho ya miaka 50 ya Bodi ya Wahandisi sambamba na Siku ya Wahandisi nchini, wahandisi 430 walikula kiapo cha utii katika taaluma hiyo ya uhandisi, ambapo jumla ya wahandisi 3,400 kutoka ndani na nje ya nchi walihudhuria maadhimisho hayo.