Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kulinda Maslahi ya Wanahabari
Jan 12, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Immaculate Makilika na Prisca Ulomi, Mwanza

Serikali imesema imedhamiria kulinda maslahi ya Waandishi wa Habari nchini kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye jijini Mwanza katika Uwanja wa Nyamagana wakati aliposhiriki katika tukio la kuaga miili ya Wanahabari 5 waliofariki katika ajali ya gari iliyotokea jana Januari 11, 2022 katika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu wakati wakielekea kwenye ziara ya kukagua miradi na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mhandisi Robert Gabriel.

Mhe. Nape amewataka waajiri wa waandishi wa habari waliofariki katika ajali hiyo kuwalipa maslahi yao kwa familia za marehemu.

"Natoa siku 7 kwa waajiri wote kuanzia leo kulipa haki za wanahabari waliofariki na taarifa za uthibitisho wa malipo ziwasilishwe kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza", alisisitiza Waziri Nape

Aidha, Waziri alisema kuwa Serikali itapitia upya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 kwa lengo la kutatua changamoto zilizopo ili kuboresha maslahi ya Wanahabari nchini.

"Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza tupitie mapungufu ya sheria hiyo na kurekebisha , mimi nitahakikisha nalinda uhuru na haki zenu, haki zenu ziko salama mikononi mwa Rais Samia, kwa kuwa sasa nimerudi nyumbani kusimamia sheria hii nitahakikisha haki zenu zinalindwa", Alisisitiza Waziri Nape

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mhandisi Gabriel alisema kuwa huu umekua msiba wa Taifa na Viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wametuma salamu za pole kwa wafiwa na wananchi wa Mkoa wa Mwanza.

Aidha, aliongeza kuwa Mkoa wa Mwanza umepata pigo kubwa na watahakikisha viongozi wa Mkoa huo wanaendelea kutoa ushirikiano kwa wanahabari nchini ili kusaidia waendelee kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

Wanahabari watano waliofariki katika ajali hiyo ni Abel Ngapemba, Afisa habari wa Mkoa wa Mwanza, Steven Msengi, Afisa habari Wilaya ya Ukerewe, Husna Milanzi mwandishi wa ITV, Johari Shani mwandishi wa Uhuru digital na Anthony Chuwa mwandishi wa kujitegemea.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi