Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kuendelea Kutoa Kipaumbele kwa Watanzania Kupata Ajira Katika Taasisi Zote Nchini
May 17, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na: Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuhakikisha Watanzania wanapewa nafasi ya kwanza kuajiriwa katika Taasisi zote hapa nchini.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Bungeni, Jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum Mhe. Leah Komanya juu ya Serikali kuchunguza na kuchukua hatua ikiwa kuna wafanyakazi wa kigeni ambao wameajiriwa katika maeneo nyeti kama vile viwanja vya ndege, bandari na kwenye mipaka ya nchi.

"Serikali imeratibu vizuri sana suala la ajira nchini. Ajira zinazotolewa kwa wageni ni kwa nafasi zile za wataalamu ambao Watanzania hawana uwezo nazo," amesema Waziri Mkuu.

Ameendelea kwa kusema, Taasisi zimepewa nafasi tano za kuajiri wafanyakazi wa kigeni kwa nafasi ambazo Tanzania hazina Wataalamu. Aidha Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu hufanya ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha kuwa Watanzania wanapewa kipaumbele katika nafasi zote wanazozimudu.

Aidha amesema, Serikali itahakikisha Watanzania wanapata fursa ya kwanza kuajiriwa katika maeneo yote nyeti kama vile bandari, uwanja wa Ndege na kwenye mipaka ya nchi ili kusiwepo na jambo lolote la kuvunjika kwa amani ya nchi.

Akijibu swali la Mbunge wa Ukonga Mhe. Mwita Waitara juu ya hatua gani Serikali imechukua dhidi ya maeneo yaliyoathirika na mvua zinazoendelea hapa nchini, Waziri Mkuu amesema ni kweli nchi imepata athari kubwa kutokana na kuwepo kwa  mvua nyingi na kusababisha barabara, nyumba na miundombinu mengine kuharibika.

Amesema kwa sasa kamati za maafa za wilaya nchini zinafanya tathimini ya uharibufu wa miundombinu katika kila wilaya ikiwemo wilaya ya Ilala.

"Kamati za maafa za wilaya zikishafanya tathimini hizo watafanya marekebisho kwa maeneo ambayo wanayamudu na kwa maeneo wasiyoyamudu watayapeleka katika kamati za maafa ngazi ya mkoa na ikiwa mkoa utashindwa basi tathimini hiyo itatumwa ofisi ya Waziri Mkuu," amesema Mhe. Majaliwa.

Amesema marekebisho ya miundombinu ya barabara itafanywa na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kwa kushirikaina na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi