Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kuendelea Kupambana na Kilimo cha Mirungi
Jun 01, 2017
Na Msemaji Mkuu

Frank Mvungi.

Serikali imetangaza kuendesha operesheni ya kuteketeza mashamba ya mirungi kote nchini ikiwa ni mkakati wa kupambana na dawa za kulevya.

Hatua hiyo inafuata baada ya kuteketeza mashamba ya bangi zaidi ya 150 yenye ukubwa wa ekari 165 katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Bw. Rogers Sianga wakati akizungumza kwenye kipindi maalum kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV.

“Dawa za kulevya zinaathiri sana nguvu kazi ya Taifa na tangu Mamlaka hii imeanza tumefanikiwa kudhibiti uingizaji wa Heroine, Cocaine na dawa nyingine za kulevya na tumewakamata wafanyabiashara wakubwa ambao walikuwa wanatafutwa na mataifa makubwa na hiyo ni hatua kubwa kwa nchi yetu katika mapambano haya” Alisisitiza Sianga.

Akifafanua Sianga alisema kuwa Serikali imepanga kuongeza vituo vya kuhudumia waathirika wa dawa za kulevya katika Mikoa ya Mbeya, Dodoma na Mwanza kwa awamu ya kwanza kutokana na mafanikio yaliyofikiwa katika kudhibiti uingizwaji wa dawa za kulevya na matumizi yake.

Mikoa mingine itakayofuata katika mpango wa kuanzishwa kwa vituo hivyo ni Pwani, Morogoro, Kilimanjaro na Arusha.

“Tumejipanga kudhibiti maeneo yote yanayotumika kupitisha dawa za kulevya katika hili tunaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa Mamlaka ili dhamira ya Serikali ya kuondoa tatizo la dawa za kulevya hapa nchini litimie.”Alisisitiza Sianga.

Akizungumzia ushirikiano na wananchi Sianga alisema kuwa kila siku wananchi 5 hadi 10 wanafika katika Mamlaka hiyo kutoa taarifa hali inayoonyesha mwamko kwa wananchi katika kupambana na dawa za kulevya katika maeneo yao na katika Taifa kwa ujumla. Katika hatua nyingine Sianga alibainisha kuwa wameanza kufuatilia Kemikali Bashirifu zinazoingizwa hapa nchini kwa kuwa zinaweza kutumika vibaya na watu wenye nia mbaya kuzalisha dawa za kulevya. “Kemikali Bashirifu zinaweza kutumika vibaya kuzalisha dawa za kulevya hivyo lazima tuzifuatilie na kudhibiti uingizwaji wake ili uzingatie sheria na taratibu na zitumike kwa makusudi chanya tu na si vinginevyo.” Alieleza Sianga. Hivi karibuni Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya nchini,kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na Mamlaka ya Chakula na Dawa TFDA,walifanikiwa kukamata shehena kubwa ya kemikali Bashirifu zinazoweza kutumika kutengeneza dawa za kulevya katika eneo la Mwenge Jijini Dar es Salaam. Aidha katika msako huo pia mfanyabiashara Benedict Assey mmiliki wa shehena hiyo alibainika kumiliki kiasi kikubwa cha kemikali hizo katika Miji ya Bagamoyo,na Moshi mkoani Kilimanjaro.          

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi