Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kuendelea Kuelekeza Fedha Katika Maeneo ya Vipaumbele
Jun 08, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_3052" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Fedha na Mpango Mhe.Dr.Philip Mpango akiwasilisha Bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2017/18.[/caption]

Na: Mwandishi Wetu

Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Mpango amewasilisha Bungeni bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/18, na kusisitiza kuwa, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa fedha zinaelekezwa kwenye maeneo ya vipaumbele ili kutekeleza kikamilifu Mpango wa Maendeleo wa Mwaka.

Katika kufanya hivyo, alibainisha kuwa Serikali itaweka mkazo katika kusimamia kwa makini nidhamu katika matumizi kwa kuhakikisha kuwa thamani ya fedha inapatikana.

Katika bajeti hiyo, Waziri Mpango amebainisha kuwa Serikali imepanga kutumia jumla ya shilingi bilioni 31,712.0 ambapo fedha kwa ajili ya maendeleo ni shilingi bilioni 11,999.6 sawa na asilimia 38 ya bajeti yote.

Kwa mujibu wa Dk. Mpango, fedha kwa ajili ya matumizi ya kawaida ni shilingi bilioni 19,712.4 ikijumuisha shilingi bilioni 7,205.8 za mishahara na shilingi bilioni 9,461.4 kwa ajili ya kulipia deni la umma na huduma nyinginezo.

Waziri Mpango ameuambia Mkutano wa 7 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa kati ya fedha hizo mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya Halmashauri yanatarajiwa kuwa shilingi bilioni 19,977.0, sawa na asilimia 63.0 ya bajeti yote, huku Serikali ikilenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya shilingi bilioni 17,106.3 sawa na asilimia 85.6 ya mapato ya ndani.

Aidha, alibainisha kuwa Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia shilingi bilioni 3,971.1 sawa na asilimia 12.5 ya bajeti yote.

Akizungumzia hatua zitakazochukuliwa na Serikali amesema kuwa ni pamoja na kusimamia nidhamu ya matumizi, kuendelea kuhakikisha kuwa Mashirika ya Umma yaliyoundwa kwa lengo la kujiendesha kibiashara, yanajiendesha kwa faida bila kutegemea ruzuku ya Serikali.

Hatua nyingine ni kuhakikisha mikataba inayoingiwa na Serikali na Taasisi zake inakuwa katika shilingi za Kitanzania isipokuwa kwa mikataba inayohusisha biashara na huduma za  kimataifa na kuendelea kudhibiti matumizi ya umeme, simu na maji ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia zinazopunguza gharama katika matumizi hayo.

Waziri Mpango alizitaja hatua nyingine kuwa ni kuendelea kudhibiti ulipaji wa mishahara kwa kulipa watumishi wanaostahili pamoja na kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kufanikisha mawasiliano katika shughuli za Serikali.

Waziri wa Fedha ameliambia Bunge kuwa dhima ya bajeti ya mwaka 2017/2018 ni “kujenga uchumi wa viwanda utakao chochea ajira na ustawi endelevu wa jamii” hivyo Serikali imejikita katika kutekeleza shabaha nane kuu.

Alizitaja shabaha hizo kuwa ni pamoja na kukuza pato halisi la Taifa kutoka asilimia 7.0 mwaka jana hadi asilimia 7.1 mwaka 2017, Kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei katika wigo wa tarakimu moja kati ya asilimia 5.0 na asilimia 8.0 mwaka 2017 na kuongeza Mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri kufikia asilimia 15.8 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17 na kuendelea kuongezeka kufikia asilimia 16.5 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18.

Shabaha nyingine ni kuinua Mapato ya kodi kutoka matarajio ya asilimia 13.3 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17 hadi kufikia asilimia 14.2 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18, kupunguza Nakisi ya bajeti kutoka asilimia 4.5 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17 hadi kufikia asilimia 3.8 ya Pato la Taifa na Kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayotosheleza mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.

Mapema asubuhi, Waziri wa Fedha aliwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2-17/2018 ambapo alieleza kuwa Tanzania ni mojawapo ya nchi chache katika bara la Afrika zilizojipambanua kwa kuwa na utulivu wa uchumi jumla kwa muda mrefu sasa.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi