Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kuendelea Kuboresha Sekta ya Anga nchini
Sep 11, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO

DODOMA

Serikali  kuendelea kujenga na kuboresha viwanja vya ndege nchi nzima ili kukuza sekta ya anga hivyo kuchochea maendeleo kwa kukuza usafirishaji kwa njia ya anga.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe wakati wa kipindi cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na  kuratibiwa na Idara ya Habari MAELEZO.

Mhandisi Kamwelwe amesema kuwa kumekuwa na ujenzi sambamba na ukarabati wa viwanja mbalimbali vya ndege nchini ikiwemo kiwanja cha ndege cha Dar es Salaam (terminal iii), ili kuweza kuwanufaisha wananchi kwa kuchochea maendeleo.

"Mpaka sasa terminal iii imefikia asilimia 80 na matarajio yetu mwezi May, 2019 unatarajiwa kukamilika na utahudumia takribani abiria milioni 6, tumekarabati uwanja wa ndege wa KIA, Mwanza, Songwe, Shinyanga, Musoma, Mtwara Songea na Rukwa, lengo ni kuwafanya wanancgi wapate huduma ya usafiri wa anga," alisisitiza Mhandisi Kamwelwe.

Akizungumza kuhusu ufungaji wa rada, Mhandisi Kamwelwe amesema kuwa Serikali imefunga rada kwatika viwanja vya ndege vya Kilimanjaro, Songwe, Dar es salaam na Mwanza zilizogharimu kiasi cha shilingi bilioni 67.5 ikiwa ni moja ya juhudi za Serikali kuimarisha usafiri wa anga nchini.

Aidha, amesema kuwa Serikali inaboresha Bandari ya Dar es Saalam kwa kuongeza gati namba 8 ambayo ujenzi wake unaendelea, lengo likiwa ni kuwa na gati 12.

"Tumeshaanza kusafirisha mizigo kwa treni kutoka Dar es Saalam hadi Mwanza baada ya hapo inachukuliwa na meli kwenda nchini Uganda" ameongeza Mhandisi Kamwelwe.

Hatahivyo Mhandisi Kamwelwe ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kuboresha Bandari zote nchini ili kuweza kuboresha sekta ya uchukuzi hapa nchini.

Kipindi cha TUNATEKELEZA kinarushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kuratibiwa na Idara ya Habari MAELEZO ambapo awamu hii inahusisha Mawaziri wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi