Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kudhibiti Mipaka 53 Isiyo Rasmi Kanda ya  Magharibi
Jun 24, 2020
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_53510" align="aligncenter" width="750"] Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe akikata utepe wakati wa hafla ya uzinduzi wa ofisi ya Shirika la Viwango (TBS) Kanda ya Magharibi itakayohudumia Mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa. Hafla hiyo imefanyika Mjini Kigoma.[/caption]

Na Mwandishi Wetu- TBS

Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara nyingine zitadhibiti mipaka isiyo rasmi 53 katika Mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa ili kukabiliana na changamoto ya uingizaji holela wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa jana mjini Kigoma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Riziki Shemdoe wakati wa hafla ya uzinduzi wa ofisi ya Shirika la Viwango (TBS) Kanda ya Magharibi itakayohudumia Mikoa ya Kigoma,Katavi na Rukwa na kwamba kwa sasa TBS ishirikiane na taasisi nyingine za Serikali katika kushughulikia suala hili wakati Wizara ikiendelea na taratibu za kupatia ufumbuzi.

Prof. Shemdoe alitoa ahadi hiyo kufuatia taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athuman Ngenya ambaye pamoja na mambo mengine alieleza uwepo wa mipaka isiyo rasmi ambayo inakwamisha juhudi za Shirika za kudhibiti uingizwaji wa bidhaa hafifu katika soko la Tanzania.

Katika taarifa hiyo Dkt. Ngenya alifafanua kuwa kati ya mipaka hiyo 53, Mkoa wa Rukwa unaongoza kwa kuwa na mipaka isiyo rasmi 35 ikifuatiwa na Kigoma 14  na Katavi mine (4).

“Suala la mipaka ni mtambuka hivyo nitawasiliana na wizara nyingine ili kupata ufumbuzi wa suala hili kwani uwepo wa mipaka isiyo rasmi pia nchi inapoteza mapato,” alisisitiza Prof. Shemdoe.

Prof Shemdoe  ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Kigoma kwa ushirikiano wanaoutoa kwa taasisi zilizopo mkoani hapa na amezitaka pia taasisi zilizo chini ya wizara hiyo pia kushirikiana na uongozi wa mkoa ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi.

“Ni imani yangu kuwa kufunguliwa kwa  ofisi ya TBS mkoani Kigoma itakuwa ni chachu ya maendeleo kwa mikoa ya Kanda ya Magharibi,” Alieleza Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe ameipongeza TBS kwa kufungua ofisi mkoani Kigoma hivyo kufanya idadi ya ofisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara mkoani Kigoma kuwa Tatu kwani Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na Wakala wa Vipimo tayari wana ofisi mkoani hapa.

Uzinduzi wa ofisi ya Kanda ya Magharibi unafanya TBS kuwa na ofisi za kanda sita (6) zikiwemo za Kanda ya Ziwa (Mwanza, Kagera, Shinyanga, Geita na Simiyu), Kaskazini (Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga), Kati (Dodoma, Singida na Tabora), Ķusini (Mtwara, Lindi na Ruvuma). Pia ofisi za Makao Makuu Dar es Salaam inafanya kazi katika mikoa iliyopo  mashariki mwa nchi yaani Dar es Salaam,  Pwani na Morogoro.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi