Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini Tanzania (TARURA), inatarajia kuanza utekelezaji wa Mradi wa Bonde la Msimbazi jijini Dar es Salaam kuanzia Jumatatu, tarehe 15 Aprili, 2024, kwa kubomoa nyumba katika eneo la Jangwani na kandokando ya mto Msimbazi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Aprili 12, 2024 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi alisema TARURA itaanza kutekeleza mradi huo kwa kuzingatia makubaliano yake na wakaazi wa eneo hilo kwamba nyumba zao zitafanyiwa tathmini; watalipwa fidia zao: na wiki sita baada ya fedha kuingizwa kwenye akaunti zao TARURA itavunja nyumba katika eneo husika.
Alisema hadi kufikia tarehe 29 Februari, 2024, TARURA ilikuwa imeshaingiza malipo ya fidia ya kiasi cha shilingi bilioni 52.61 kwenye akaunti za wamiliki wa nyumba wapatao 2,155 kati ya 2329 walioandikishwa katika daftari la kwanza ambapo hivi sasa inakamilisha malipo ya fidia kwa wahusika wengine 446 waliomo kwenye daftari la pili ambao hawakufanyiwa uthamini wa awali kwa sababu mbalimbali.
“TARURA itashirikiana na ofisi za Halmashauri za mkoa wa Dar es Salaam katika maeneo ambapo mradi unapita ili kuhakikisha kazi inafanyika kwa usahihi na umakini. Mradi wa Bonde la Msimbazi umelenga kupunguza athari za mafuriko; kuongeza matumizi bora ya ardhi; kuzuia mmomonyoko wa udongo; kurejesha uoto wa asili; kuruhusu maji ya mto yaende baharini; na utunzaji wa maji,” alisema Matinyi.
Alisema kwamba hadi kukamilika kwake, mradi huu itachukua miaka mitano hadi mwaka 2028 na utagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 260 sawa na shilingi bilioni 675 ambazo zitatumika kujenga miundombinu ya kukabiliana na mafuriko: ujenzi wa karakana ya mabasi ya mwendokasi kwenye eneo la Ubungo Maziwa baada ya kuihamisha kutoka Jangwani; ujenzi wa daraja la Jangwani; ujenzi wa bustani ya jiji na uendelezaji wa maeneo ya makazi na biashara; kupanua mto Msimbazi na kuuongeza kina: pamoja na usimamizi wa taka ngumu.
Akijibu swali la mwandishi aliyetaka kujua ni muda gani zoezi la kubomoa litatumia hadi kukamilika kwake, Mratibu wa Miradi ya Benki ya Dunia, Mhandisi Humphrey Kanyeye alisema wanatarajia zoezi hilo litakamilika ndani ya miezi mitatu (3) hii kutokana na kukamalisha zoezi la malipo kwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo ambao bado walikuwa kwenye mchakato wa malipo pamoja kushughulikia masuala yote yatakayojitokeza.
Alisema TARURA itaendesha zoezi la kubomoa kwa kushirikisha taasisi nyingine kama vile Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASA) aidha, TARURA inawashauri wananchi watakaokuwa na maswali kuhusu zoezi hili kupiga simu nambari 0738-353854 au 0738-353855 iwapo watahitaji ufafanuzi wowote.