Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kuwekeza kwenye sekta za elimu na afya ili kutatua changamoto za kijamii ambapo kati ya mwaka 2021 hadi 2023, sekta hizo zimeendelea kufanya vizuri nchini.
Rais ameyasema hayo leo Oktoba 29, 2024, wakati akifungua mkutano wa 11 wa taasisi ya Merck, unaoendelea Jijini Dar es Salaam ambao unalenga kujadili na kutafuta suluhu dhidi ya changamoto mbalimbali za afya na kijamii zinazokabili bara la Afrika na Asia.
“Ninajua kuwa Taasisi ya Merck ina maslahi makubwa katika nyanja za afya na elimu, na hivyo kutambua dhamira hii, Serikali yangu imeweka kipaumbele kwenye sekta hizi ikiwemo afya ya mama na mtoto, mimi mwenyewe toka nikiwa Makamu wa Rais na sasa ni Rais niliweka kipaumbele cha kuboresha afya ya mama na mtoto nchini, kati ya mwaka 2021 hadi 2023 tuliongeza mafanikio katika huduma za afya kwa kujenga na kuendeleza zaidi ya hospitali 127 za wilaya na zaidi ya vituo 367 vya huduma za afya nchini kote.” Amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema kutokana na afua mbalimbali, utafiti wa idadi ya watu na afya wa mwaka 2022, unaonyesha kuwa vifo vya uzazi vimepungua kutoka 556 hadi vifo 104 kati ya vizazi hai 100,0000 kwa mwaka 2015, na kushuka kwa zaidi ya asilimia 80.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum, Dkt. Doroth Gwajima amesema katika mkutano huo kutakuwa na mijadala ya kisayansi kuhusu kupambana na magonjwa ya afya ya uzazi, sukari na aina mbalimbali ya saratani ambazo huathiri wanawake kwa kiasi kikubwa.
Amesema Tanzania imeweka mazingira mazuri ya kisera na kisheria katika kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana ikiwemo sera ya Taifa ya jinsia ya maendeleo ya wanawake ya mwaka 2023 inayolenga kuboresha maisha ya watu wa kundi hilo, programu ya elimu kwa wasichana na uwezeshaji wanawake kiuchumi kazi ambayo imewezeshwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Nae Mwenyekiti wa Bodi wa Taasisi ya Merck Profesa, Daktari Frank amesema mkutano huo wenye mijadala mbalimbali ambayo pia imewakutanisha wake wa marais wa nchi mbalimbali, ni kubadilishana wa uzoefu na kupeana hadithi za mafanikio katika kushughulikia changamoto za huduma za afya zilizopo, kuondoa unyanyapaa na kusaidia elimu ya wasichana katika nchi zao ambazo zinashirikiana na taasisi hiyo.
Mkutano huo wa 11 wa Merck Foundation unafanyika kwa siku mbili Jijini Dar es Salaam ambao umeanza leo Oktoba 29, 2024 na umehudhuriwa na washiriki zaidi ya 700 na wake wa Marais 15 kutoka katika nchi mbalimbali Duniani.