Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Inatekeleza Miradi ya Maji yenye Thamani ya Shilingi Trilioni 5
Oct 19, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na; Frank   Mvungi

Waziri wa Maji, mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa, amesema serikali ya awamu ya tano inatekeleza miradi ya maji yenye thamani ya shilingi trilioni tano kote nchini.

Akizungumza katika kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa na runinga ya TBC1, Profesa Mbarawa amesema kiasi hicho cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya miradi hiyo inaonyesha nia ya serikali kuhakikisha Watanzania walio wengi wanapata maji safi na salama ifikapo mwaka 2020.

“Kufikia mwaka 2020 upatikanaji wa maji katika miji mikuu ya mikoa utakuwa asilimia 95, miji mikuu ya wilaya asilimia 90 na vijiji asilimia 85” amenukuliwa Profesa Mbarawa.

Akizungumzia hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakamilika kwa wakati na kutekelezwa kwa ubora unaotakiwa, Profesa Mbarawa amesema kuwa watumishi  wote wasio waaminifu wameondolewa kwenye nyadhifa zao na kwa  sasa wizara yake imejipanga vyema kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

Mbali na upatikanaji wa maji safi na salama kwenye maeneo yote nchini, Profesa Mbarawa pia amewahakikishia wakazi wa maeneo ambayo miradi mikubwa ya maji inapita watanufaika na miradi hiyo. “Katika mradi wa maji yanayotoka ziwa Victoria hadi Shinyanga, Nzega hadi Tabora tutahakikisha kuwa wananchi walio karibu na maeneo yanayopitiwa na mradi huo wanaunganishwa na huduma ya maji”

Kukamilisha mradi huo mkubwa wa maji Serikali inatumia Bilioni 600 na unatarajiwa kuwanufaisha wakazi wa mikoa ya  Shinyanga na Tabora, alisisitiza Profesa Mbarawa.

Miradi mingine mikubwa inayotekelezwa na serikali ni pamoja na mradi wa maji wa Arusha unaogharimu Bilioni 429 na utekelezaji wake unaendelea vizuri hali itakayosadia kuongeza na kutatua kabisa changamoto ya maji katika Jiji hilo la kitalii.

Akifafanua zaidi Profesa Mbarawa amesema mradi mwingine mkubwa unaotekelezwa na serikali ya awamu ya tano ni ule wa Mwanga, Same, hadi Korogwe unaogharimu bilioni 239. Kwa maelezo ya Profesa Mbarawa mradi huo utasaidia kwa kiwango kikubwa kutatua changamoto ya maji katika maeneo hayo.

Kuhusu ubora wa maji, Profesa Mbarawa awewahakikishia Watanzania kuwa yana ubora wa kimataifa na lengo la serikali kuhakikisha inaendelea  kuwapatia wananchi wote huduma ya maji safi na salama popote pale walipo.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi