Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali imewataka wafanyabiashara wa kemikali nchini kujali na kuthamini afya za watanzania
Mar 20, 2018
Na Msemaji Mkuu

Mkemia Mkuu wa Serikali Prof. Samwel   Manyele akisisitiza jambo wakati akifungua mafunzo ya siku tano kwa Wasambazaji  na Wauzaji wa Kemikali (hawapo pichani) kutoka Mikoa ya  Morogoro, Dodoma, Singida na Tabora mapema leo mjini Dodoma.

Meneja wa Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Mashariki Bw. Daniel Ndiyo (katikati) akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tano kwa Wasambazaji  na Wauzaji wa Kemikali (hawapo pichani) kutoka Mikoa ya  Morogoro, Dodoma, Singida na Tabora mapema leo mjini Dodoma.

Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya siku tano kwa Wasambazaji, Wahifadhi, Wasafirishaji  na Wauzaji wa Kemikali (hawapo pichani) kutoka Mikoa ya  Morogoro, Dodoma, Singida na Tabora yanayofanyika  mjini Dodoma kuanzia leo machi 20, hadi machi 23, 2018.

Na Beatrice Lyimo- MAELEZO, DODOMA

Serikali imewataka Wafanyabiashara wakubawa wa kemikali nchini kujali na kuthamini afya za watanzania na mazingira kwa ujumla ili kuchochea dhana ya matumizi sahihi ya kemikali.

Hayo yamesemwa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele  leo mjini Dodoma wakati akifungua mafunzo kwa wadau wa kuhifadhi, kusafirisha na kuuza kemikali yaliyolenga udhibiti na usalama wa kemikali.

“Mkiwa kama wafanyabiashara wakubwa msije mkathamini sana biashara zenu katika shughuli zenu zinazohusuhu masuala mbalimbali ya kemikali bali mjikite katika kuthamini afya za watanzania na mazingira yetu kwani ni kosa kisheria, hivyo endapo mtakwenda kinyume na taratibu mtaadhibiwa kulingana na mitaji yenu, niwaombe sana kuwa makini na mtangulize maslahi ya watanzania kwanza” alisisitiza Prof. Manyele

Aidha, Prof. Manyele amewataka wasafirishaji wa kemikali nchini kuwa na cheti cha usajili  pindi wasafirishapo kemikali  kutoka eneo moja hadi jingine kwani Sheria inaagiza hivyo ili kuchochea matumizi sahihi ya kemikali.

“Ni muhimu kwa wasafirishaji wote wa kemikali kuwa na vyeti husika kwenye magari pindi wanaposafirisha kemikali ikiwa ni utambulisho kuwa wamepitia mafunzo mbalimbali yanayotolewa na mamlaka hiyo hasa yanayosusu kanuni za usafirishaji salama wa kemikali”. Alisisitiza Prof. Manyele.

“Mpaka sasa takribani taasisi 3000 zimesajiliwa na Serikali hivyo nizidi kutoa wito kwa makampuni mengine kuzidi kujisajili kwenye mamlaka husika ili kuweza kuwa na matumizi salmama ya kemikali nchini” aliongeza Prof.  Manyele.

Vilevile Prof. Manyele amesema kuwa Serikali inaendelea kusisitiza kufuata sheria bila shuruti na kufuata taratibu zilizoanishwa kisheria juu ya matumizi na usalama wa kemikali.

Mafunzo hayo kwa wadau wa kemikali katika Kanda ya Kati ni muhimu kwani kumekuwa na mbinu mbalimbali zinabadilika kuhusu matumizi ya kemikali.

         

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi