Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Imepiga Hatua Kiuchumi, Kidemokrasia na Utawala Bora
Apr 04, 2024
Serikali Imepiga Hatua Kiuchumi, Kidemokrasia na Utawala Bora
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (kulia), akisalimiana na kiongozi wa ujumbe kutoka Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (Millennium Challenge Corporation-MCC), Bw. Nilan Fernando, jijini Dodoma, ambapo walijadiliana maeneo mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Shirika hilo ambalo limeichagua Tanzania kuwa moja ya nchi zitakazonufaika na ruzuku zinazolenga kusaidia mageuzi ya kisera na kitaasisi ili kutatua vikwazo vya ukuaji wa uchumi, rasilimali watu, demokrasia na utawala bora.
Na Peter Haule na Josephine Majura, WF, Dodoma

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amesema Tanzania itaendelea kuwekeza fedha kwenye sekta za uzalishaji, kudumisha demokrasia na utawala bora ili kukuza uchumi wa nchi na ustawi wa jamii.

 

Dkt. Nchemba ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (Millennium Challenge Corporation-MCC), jijini Dodoma waliopo nchini kwa ajili ya kufanya tathimini ya masuala mbalimbali baada ya Shirika hilo kuichagua Tanzania kuwa moja ya nchi zitakazonufaika na ruzuku zinazolenga kusaidia mageuzi ya kisera na kitaasisi ili kutatua vikwazo vya ukuaji wa uchumi, demokrasia, utawala bora na maendeleo ya rasilimali watu.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akizungumza wakati wa Mkutano wake na ujumbe kutoka Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (Millennium Challenge Corporation-MCC), ulioongozwa na Bw. Nilan Fernando, jijini Dodoma, ambapo walijadiliana maeneo mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na shirika hilo ambalo limeichagua Tanzania kuwa moja ya nchi zitakazonufaika na ruzuku zinazolenga kusaidia mageuzi ya kisera na kitaasisi ili kutatua vikwazo vya ukuaji wa uchumi, demokrasia, rasilimali watu na utawala bora.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeongeza bajeti ya sekta ya kilimo, mifugo na sekta nyingine ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao na bidhaa kwa ajili ya mauzo nje ya nchi ili kukuza uchumi na kipato cha mtu mmoja mmoja.

 

Aidha, Dkt. Nchemba aliueleza ujumbe huo kuwa Tanzania, imepitisha mkakati wa kuongeza mauzo nje ya nchi pamoja na mkakati wa kuvutia uwekezaji ambao umelenga kukuza mauzo hayo nje ya nchi na kuchangia kukuza ajira kwa vijana. 

 

“Mauzo nje hayataongezwa bila kuongeza uzalishaji, hivyo mkakati wa kuongeza mauzo nje umezilenga sekta za uzalishaji zikiwemo za kilimo, mifugo, maliasili pamoja na sekta nyingine wezeshi”, alisema Dkt. Nchemba.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (Kulia), akiteta jambo na Kiongozi wa Ujumbe kutoka Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (Millennium Challenge Corporation-MCC), Bw. Nilan Fernando, baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Shirika hilo na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba  (hayupo pichani), ambapo walijadiliana maeneo mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Shirika hilo ambalo limeichagua Tanzania kuwa moja ya nchi zitakazonufaika na ruzuku zinazolenga kusaidia mageuzi ya kisera na kitaasisi ili kutatua vikwazo vya ukuaji wa uchumi, demokrasia, rasilimaliwatu na utawala bora.
 

Alisema kuwa mkakati huo umepitishwa na Baraza la Mawaziri chini ya uenyekiti wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na umejumuishwa katika bajeti mpya ya mwaka 2024/2025 ili utekelezaji wake uweze kuanza mara moja.

 

Kuhusu masuala ya kukuza demokrasia, utawala bora na kuendeleza rasilimali watu, Dkt. Nchemba alibainisha kuwa falsafa ya R4 ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo na utulivu wa nchi ambao ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi na maridhiano ya kisiasa. 

 

Vilevile alieleza kuwa Mhe. Rais ameendelea kufanya mabadiliko yanayogusa Sera za Kikodi, biashara, utawala bora, haki za binaadamu pamoja na mazingira bora ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na Bunge kufanya rejea ya baadhi ya Sheria ili kuweka mazingira bora ya uwekezaji na biashara katika ustawi wa wananchi. 

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (wa nne kushoto mstari wa mbele) na Kiongozi wa Ujumbe kutoka Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (Millennium Challenge Corporation-MCC), Bw. Nilan Fernando (wa tatu kushoto mstari wa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa pande zote mbili baada ya kumalizika kwa Mkutano wao ambapo walijadiliana maeneo mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Shirika hilo ambalo limeichagua Tanzania kuwa moja ya nchi zitakazonufaika na ruzuku zinazolenga kusaidia mageuzi ya kisera na kitaasisi ili kutatua vikwazo vya ukuaji wa uchumi, demokrasia, rasilimaliwatu na utawala bora. Wengine katika picha ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (wa tatu kulia), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya (wa pili kulia), Mratibu wa Mradi wa MCC nchini Tanzania, Dkt. Hamisi Mwinyimvua (wa pili kushoto mstari wa mbele).

Dkt. Nchemba alisema kuwa mambo yaliyotekelezwa yameleta matokeo chanya ambapo Taasisi ambazo hutumika kufanya tathmini ya uwezo wa nchi kukopesheka katika masoko ya kimataifa, ikiwemo Taasisi ya Kimataifa ya Moody’s ambayo hivi karibuni imeipandisha Daraja Tanzania kutoka Daraja B2 with positive outlook hadi Daraja la B1 with Stable Outlook na kuwa nchi iliyofanya vizuri zaidi katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika-SADC.  

 

Akizungumzia uwezeshaji wa kifedha kwa biashara ndogo ndogo, Dkt. Mwigulu alisema kuwa tayari Mhe. Rais ametoa maelekezo ya mikopo ya vijana, wanawake na makundi maalumu kurejeshwa ikiwa imeboreshwa katika usimamizi wake ili kuwezesha watu wengi zaidi kupata fedha hizo.

  

Kwa upande wake, Kiongozi wa ujumbe huo kutoka Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC), Bw. Nilan Ferdinando, alisema kuwa Shirika lake linafurahishwa na hatua kubwa zinazochukuliwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kusimamia uchumi wa nchi, masuala ya demokrasia, haki za binadamu na utawala bora.

 

Alisema kuwa hali hiyo italifanya shirika lake kurejesha mradi wa Compact uliositishwa mwaka 2013 ambao utaiwezesha nchi kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

 

Alisema kuwa timu yake itakuwepo nchini na kukutana na makundi katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta binafsi kwa ajili ya kufanya tathimini kwa ajili ya mpango wake mpya kwa Tanzania wa kuipatia ruzuku kwa ajili ya kuboresha sera mbalimbali zitakazochangia ukuaji wa uchumi, demokrasia, utawala bora na haki za binadamu.

 

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, Mratibu wa Mradi wa MCC nchini Tanzania, Dkt. Hamisi Mwinyimvua pamoja na viongozi waandamizi wa Wizara.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi