Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Imejipanga Kuhakikisha kuwa Mifuko Mbadala ya Plastiki Inapatikana kwa Wingi ili Kukidhi Mahitaji.
Apr 10, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_42057" align="aligncenter" width="900"] Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akiongea na waandishi wa Habari kufafanua tamko la Serikali la kupiga marufuku uzalishaji, usambazaji na matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini. Mkutano huo umefanyika hii leo katika jengo la PSSSF jijjini Dodoma.[/caption]

Na Lulu Mussa

Dodoma

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika hii leo Jijini Dodoma na kusisitiza kuwa katazo la Mifuko ya Plastiki lililotolewa jana na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa linakuwa na nguvu kisheria kwa kuandika kanuni za katazo ya mifuko ya plastiki zitakazotangazwa katika gazeti la Serikali chini ya Sheria ya Mazingira na kutoa adhabu kwa kila mtu atakaekiuka utaratibu uliowekwa.  

“Kabla ya Serikali kutangaza hatua ya kupiga marufuku mifuko ya plastiki, ulifanyika utafiti na maandalizi ya mifuko mbadala. Uwezo wa kuzalisha upo na mifuko ya karatasi inayotumika Kenya na Rwanda inatumia malighafi inayozalishwa Mgololo-Iringa,Tanzania.” Makamba alisistiza

Waziri Makamba ameainisha kuwa kuna vifungashio ambavyo havitapigwa marufuku ambavyo ni pamoja na vifungashio vya dawa za hospitalini, vifungashio katika sekta ya kilimo na ujenzi pia vile vya kuhifadhi maziwa na kutolea mfano wa vifungashio vya maziwa ya ASAS na Tanga Fresh, hata hivyo utaratibu maalumu utawekwa kwa wamiliki wa kukusanya vifungashio hivyo mara baada ya matumizi yake.

Akizungumzia juu ya ushirikishwaji, Waziri Makamba amesema kuwa zoezi hili limekuwa ni shirikishi na hatua iliyotangazwa na Waziri Mkuu sio ya kushtukiza kwa kuwa Ofisi yake iliratibu mikutano katika maeneo kadhaa nchini kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu zuio la mifuko ya plastiki.

Katika kukamilisha utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Waziri Makamba amesema Ofisi yake imeunda kikosi kazi cha kusimamia katazo hilo kikihusisha wajumbe kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Shirika la Viwango Tanzania, Mamlaka ya Chakula na Dawa, Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Wengine ni Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Katika hatua nyingine Waziri Makamba amesema kuwa mapema wiki ijayo ataitisha mkutano wa wawekezaji wa mifuko mbadala kote nchini na kujadili kwa kina namna bora ya kuwekeza katika uzalishaji wa mifuko mbadala rafiki wa mazingira.

Serikali imetangaza kuanzia Juni Mosi 2019 kuwa ni marufuku kutengeneza, kuingiza, kuuza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote na matumizi yake.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi