Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Sera ya Ardhi Iliyoboreshwa Kuweka Mfumo Madhubuti Matumizi ya Ardhi
Mar 17, 2025
Sera ya Ardhi Iliyoboreshwa Kuweka Mfumo Madhubuti Matumizi ya Ardhi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria uzinduzi wa magari 70 yatakayogawiwa kwa Maafisa Ardhi wa Mikoa na Halmashauiri ili kutekeleza kazi za wizara kwa ufanisi. Uzinduzi huo umefanyika leo Machi 17, 2025 jijini Dodoma ukiambatana na uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995 (Toleo la 2023).
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995 (Toleo la 2023) iliyozinduliwa leo Machi 17, 2025 jijini Dodoma ina lengo la kuhakikisha nchi inakuwa na mfumo madhubuti na wenye usawa wa umiliki, upatikanaji na usimamizi wa matumizi ya ardhi kwa maendeleo endelevu.

Rais Samia amesema hayo leo wakati akizindua Sera hiyo inayoratibiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambapo pamoja na mambo mengine, amewahakikishia Watanzania kuwa misingi iliyowekwa kwenye Sera ya Ardhi ya mwaka 1995 haijabadilishwa.

“Ardhi itaendelea kuwa mali ya umma na Rais ndiyo mdhamini kwa niaba ya wananchi wote, haki ya kumiliki na kutumia ardhi iliyopatikana ama kwa kumilikishwa au serikali au kimila itaendelea kuwa mifumo pekee ya kumiliki ardhi, tulichokiondoa ni mila potofu ya kwamba mwanamke hawezi kumiliki ardhi”, amesema Rais Samia.

Rais ameongeza kuwa, Kamishna wa Ardhi ataendelea kuwa na Mamlaka ya kipekee ya utawala wa ardhi nchini na raia wa Tanzania pekee ndiyo wenye haki ya kumiliki ardhi huku wasio raia wana haki ya kutumia ardhi kwa kukodishwa, hiyo ndiyo misingi inayowahakikishia Watanzania ustawi kupitia rasilimali ya ardhi.

Ameyataja masuala sita yaliyopo katika sera hiyo ikiwemo kuyajumuisha na kuyapa msingi wa kisera masuala muhimu ambayo hayakuwa yamezingatiwa kwenye sera iliyopita ikiwemo zoezi la uimarishaji wa mipaka ya kimataifa ya Tanzania na nchi jirani, kubainisha haja ya kuweka utaratibu wa kisera wa kusimamia uchumi wa rasilimali zilizopo kwenye maji kwa kupima na kumilikisha ardhi hizo pamoja na kujumuisha lengo la kuimarisha usimamizi wa soko la ardhi nchini.

Vilevile, Sera itaimarisha uthamini na ulipaji wa fidia, itaimarisha uwekezaji katika uendelezaji wa ardhi na kusaidia katika kukabili migogoro ya ardhi kwa kutumia TEHAMA pamoja na kuzingatia hoja za muda mrefu za Diaspora wa Tanzania kuhusu kuwa na haki ya kutumia ardhi yao ya Tanzania.

Ameipongeza, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wataalam na wadau walioshiriki kufanikisha kuandaliwa kwa sera hiyo pamoja na mabadiliko makubwa yaliyofanyika chini ya wizara hiyo kutoka kuwa Wizara ya migogoro, uzembe wa makusudi hadi kuwa Wizara ya maendeleo ya watu.

Kwa upande wake Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi amesemaSera hiyo inayozinduliwa leo inaendana na hali halisi na nyakati za sasa ambapo imeziweka kando mila na desturi zilizopitwa na wakati katika masuala ya ardhi.

"Pamoja na hayo,  tunashukuru kwa fedha zaidi ya dola za Marekani milioni 65 ulizotoa kwa ajili ya kutengeneza upya ramani ya nchi yetu ambapo ikifika mwaka 2030, Wizara itakuwa imetekeleza agizo lako la kupima nchi yote na kuipanga kulingana na mahitaji ya eneo husika.” Amesema Mhe. Ndejembi.

Mhe. Ndejembi amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuwapatia magari kwa ajili ya maafisa yatakayowarahisishia kufika hadi kwenye Halmashauri na mikoa ili kuhakikisha watumishi wa Wizara ya Ardhi wanatekeleza majukumu yao kwa weledi na kwa wakati kwa wananchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi