Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rushwa Yapungua, Huduma Zaimarika - Afrobarometer
Feb 07, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Wetu

Utafiti uliofanywa na taasisi ya Afrobarometer kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti na Kupambana na Umasikini (REPOA) imeonesha ongezeko la wananchi kuridhishwa na utoaji wa huduma muhimu nchini.

Katika taarifa yake ya Januari 2019 kuhusu mtazamo wa wananchi juu ya huduma zinazotolewa na Serikali katika sekta za afya, maji, elimu na umeme, imeonesha ongezeko la wananchi kuridhishwa na upatikanaji wa huduma hizo nchini.

Katika sekta ya afya, asilimia 54 ya wananchi waliohojiwa wameonyesha kuridhishwa na upatikanaji wa huduma hizo ikiwa ni ongezeko la asilimia 8 ukilinganisha na utafiti kama huo uliofanywa mara ya mwisho mwaka 2014. Aidha, asilimia 58 ya wananchi wamesema wanaridhishwa na maboresho yaliyofanywa na Serikali katika sekta ya afya ikiwa ni ongezeko la asilimia tisa.

Vita dhidi ya rushwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano imeonesha kuzaa matunda ambapo ripoti hiyo inasema kuwa asilimia 89 ya wananchi walipata huduma za afya bila ya kutoa rushwa, kuridhishwa huku kwa wananchi ni sawa na ongezeko la asilimia 10 ukilinganisha na mwaka 2014.

Kuhusu mtazamo wa wananchi kwenye upatikanaji wa huduma za maji safi, maji taka na umeme ripoti inaonesha ongezeko la asilimia 15 wakati vitendo vya rushwa katika maeneo hayo vikipungua kwa zaidi ya nusu kutoka asilimia 20 mwaka 2014 hadi asilimia nane mwaka 2017.

Kwa mujibu wa Afrobarometer, wananchi tisa kati ya 10, sawa na asilimia 92 ya waliohojiwa wamesema hawakuwahi kutoa rushwa kupata huduma za maji safi, maji taka na umeme, wakati asilimia 48 sawa na ongezeko la asilimia nne wameonyesha kuridhishwa na namna Serikali inavyoshughulikia masuala ya maji safi, maji taka na umeme.

Mtazamo wa wananchi kwenye sekta ya elimu vilevile umeendelea kuonyesha taswira chanya ambapo ripoti hiyo imeonyesha zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wanaridhishwa na upatikanaji wa huduma zinazotolewa na shule za umma ikiwa ni ongezeko asilimia 12.

Aidha, asilimia 96 ya wananchi walisema hawakuwahi kutoa rushwa katika kupata huduma za shule za umma ikiwa ni ongezeko la asilimia tisa. Kuhusu kuridhishwa na namna Serikali inavyo shughulikia masuala ya elimu, asilimia 73 ya wananchi wameonyesha kuridhishwa ukilinganisha na asilimia 54 ya mwaka 2014.

Afrobarometer ni mtandao wa taasisi za utafiti uliopo katika nchi zaidi ya 35 barani Afrika. Kwa mujibu wa taarifa zinazopatikana kwenye tovuti yake Afrobarometer inajinasibu kama mtandao wenye mrengo wa kiafrika na usiofungamana na itikadi za kisiasa ambao umebobea kwenye tafiti za kupima mitizamo ya wananchi kwenye eneo la demokrasia, utawala na hali ya uchumi kwa miaka ishirini sasa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi