Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Marufuku Wanafunzi Kuvuna Mazao wakati wa Masomo
May 03, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Tiganya Vincent - RS Tabora

SERIKALI imesema itawachukulia hatua watu wote ambao watakutwa wakiwatumia watoto kuvuna pamba, tumbaku, mpunga na mazao mengine jambo linalosababisha kuwa watoro na kushindwa kuhudhuria masomo.

Kauli hiyo ilitolewa jana Wilayani Igunga na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati akiongea na Maafisa Watendaji wa Kata, Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule na Walimu wakuu.

Alisema vitendo vya kuwatumia watoto kipindi hiki katika kazi mashambani limechangia Mkoa wa Tabora kuwa miongoni mwa maeneo hapa nchini yanayoongoza kwa utoro na mimba za utotoni.

Kufuatia kuwepo kwa vitendo vya utoro Mwanri aliwaagiza viongozi wote kuanzia ngazi za vitongoji kushirikiana na walimu kukabiliana na utoro ambao unarudisha nyuma maendeleo ya watoto na maendeleo ya Mkoa wa Tabora.

Mwanri alisema hatasita kumchukulia hatua kiongozi wa ngazi yoyote kuanzia Kijiji au kitongoji na walimu ambao watashindwa kutekeleza wajibu wao katika kukomesha utoro.

“Kila mtu ni lazima asimame katika nafasi yake ukiwa mwalimu hakikisha unafuatilia mahudhurio na kwa wale watoro majina yao yapelekwe kwa Mtendaji wa Kata kwa ajili ya kumchukulia hatua na nakala ya barua hiyo ipelekwe kwa Wakuu wa Wilaya” alisema Mwanri.

Alisema walimu wakuu na Wakuu wa Shule wanapaswa kuhakikisha kila siku wanachukua orodha ya mahudhurio na kupeleka majina ya watoto watoro na wazazi wao kwa Watendaji wa Vijiji na Kata ili waweze kuchukuliwa hatua.

Mwanri alisema kwa Watendaji nao wanapaswa kufuatilia watoto ambao hawahudhurii shule na kuwapeleka Mahakamani Wazazi wao kama Waraka wa Elimu wa Mwaka 2002 unavyoagiza.

Naye Katibu Tawala Mkoa Msaidizi anayeshughulikia Elimu Suzan Nussu aliwataka Maafisa Elimu Kata na Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu kuhakikisha wanafunzi wote waliondikishwa kujiunga na masomo wanafanya mitihani yao ya kuhitimu  darasa la saba na wale wa Sekondari wanahitimu Kidato cha Nne.

Alisema hatua hiyo itausaidia Mkoa wa Tabora kuondokana na aibu ya kuwa miongoni mwa Mikoa inayoongoza kwa utoro.

Mdhibiti Mkuu wa Ubora wa Shule Kanda ya Magharibi, Alvini Mugasha aliwataka wanajamii wanapomuona mwanafunzi akiwa  nje ya mazingira ya shule wakati wa masomo wamkemee.

Alisema kuwa ni jukumu la walimu kuhakikisha wanachukua orodha ya mahudhurio na kutoa taarifa katika Mamlaka husika ili wazazi wa watoro wachukuliwe hatua za kisheria.

Mapema mwezi uliopita Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa Magogo mkoani Geita aliitaja  mikoa ya Tabora, Geita, Mtwara na Shinyanga kuwa inaongoza kwa utoro wa wanafunzi wa sekondari.

Aliongeza kuwa mikoa ya Rukwa, Geita, Tabora, Singida na Simiyu kuwa inaongoza kwa utoro wa wanafunzi wa shule za msingi.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi