Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RC Tabora Atoa Wiki Moja kwa Halmashauri ya Sikonge na Polisi Kujenga Vituo katika Eneo la Kitunda.
May 26, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Tiganya Vincent – RS Tabora.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri ametoa siku saba kwa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge na Jeshi la Polisi kujenga mahema katika eneo la Kitunda kwa ajili kuwasogezea huduma ya afya na ulinzi kwenye makazi ya wachimbaji wadogo wadogo na wafanyabiashara waliopo katika eneo hilo.

Hatua hiyo inalenga kuwaepusha wakazi hao na madhara ambayo yanaweza kuwapata kutokana na kukosekana kwa huduma ya upimaji , tiba na ulinzi katika eneo hilo.

Bw. Mwanri alitoa kauli hiyo jana wilayani Sikonge kwenye Mkutano wa hadhara uliowahusisha wachimbaji wadogo wadogo , Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge,Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya ya Sikonge na viongozi wa Kampuni zenye leseni ya uchimbaji wa madini  katika eneo la Kitunda.

Alisema kuwa idadi ya watu wanaoishi katika eneo hilo ni kubwa , hivyo ni vema wakasogezewa huduma za afya karibu kwani wao nao wanahaki ya kupata matibabu mazuri kama walivyo wananchi wengine walioko maeneo meninge ya  uzalishaji.

Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza kuwa jengo la Afya lisio lazima lijengwe kwa kutumia matofali bali Halmashauri inaweza kutumia maturubai ambayo yagawanywa katika vyumba mbalimbali vya utoaji tiba na vipimo ili wachimbaji hao waache kumeza dawa ovyo bila ushauri wa wataalam.

Mkuu wa Mkoa pia alisisitiza kuwa huduma hiyo ni muhimu kuwa karibu vijana wanaojihusisha na uchimbaji madini kwa sababu uimara wa afya zao ni muhimu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Aidha ,Bw. Mwanri alitoa wito kwa wachimbaji hao wadogo wadogo kujiunga na Mfuko wa Huduma ya Afya ya Jamii ili waweze kupata huduma za afya gharama nafuu kuliko kutegemea zaidi malipo ya papo kwa papo.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa alimwagiza Kamanda wa Polisi Wilaya Sikonge kuweka Hema kwa ajili ya Kituo cha Polisi Kidogo katika eneo hilo ili kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao.

Alisema kuwa Polisi wawe wanafanya doria kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayenyanyaswa na wenzake wakati akiendelea na shughuli za kujiingizia kipato na kulinda wafanyabiashara wasivamiwe.

Mkuu huyo Mkoa aliongeza kuwa ni vema Polisi wawe wanafanyakazi kwa kubadilishana ili kuepuka kujenga mazoea ya wachimbaji hao na hivyo kuathiri utendaji wao.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi