[caption id="attachment_33358" align="aligncenter" width="750"] Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akitoa elimu jana kwa Wanakijiji wa Bukoko wilayani Igunga ikiwa ni sehemu ya kampeni yake ya kutaka wananchi ambao sio watumishi kujiunga na mfuko huo.[/caption]
NA TIGANYA VINCENT - RS TABORA
SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imetoa miezi miwili kwa Mwekezaji wa Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya TAURTZ Limited- Nanga wilayani Igunga kuhakikisha analipa deni la milioni 43.4 ambazo alipaswa kuziwasilisha katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka huu ikiwa ni stahiki ya michango ya kila mwezi ya wafanyakazi kwenye mfuko huo.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini Igunga na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa kikao maalumu cha Chama Kikuu cha Ushirika cha Igembensabo.
Alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Igunga kuwakutanisha viongozi wa kampuni ya uchimbaji madini TAURTZ Limited- Nanga na wale wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili wapange namna ya kulipa deni hilo haraka na kutoa mpango kazi na muda wa kulipa deni hilo na kama ataendelea kukaidi atalazimika kukamata mali za Kampuni hiyo ili ziweze kufidia deni hilo.
Mwanri alisema tabia za namna hiyo ndizo zimekuwa zikisababisha haki za wafanyakazi wanapostaafu kupotea na kama amefariki wale warithi kukosa kwa sababu ya michango yake kutowasilishwa katika Mifuko wa Hifadhi ya Jamii.
“Mimi nikiwa msimamizi wa shughuli zote za Serikali siwezi kukubaliana na waajiri wote ambao hawapeleki makato ya watumishi katika mifuko ya hifadhi ya jamii ndio maana baadhi ya waastafu wamekuwa wakipata taabu wanapokwenda kuchukua kiinua mgongo cha na ikitokea bahati mbaya akafariki hata wale warithi wanakosa haki za ndugu yao kwa hilo siwezi kukubali nitaweka mguu wangu chini hadi kieleweke” alisema.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa huyo amemwagiza Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) wilayani Igunga kuichunguza kampuni hiyo kuona kama kweli inalipa kodi za Serikali zinastahili na kuongeza kuwa kitendo cha kukaidi kupeleka michango ya wafanyakazi upo uwezekano wa kukuta hata kodi hawalipi licha ya kuendesha shughuli za uchimbaji madini katika eneo hilo.
Kwa upande wa Meneja wa NSSF kwa upande wa Wilaya ya Igunga na Nzega, Shimo Mussa alisema viongozi wa Kampuni hiyo wameshindwa kuwalisha michango ya wafanyakazi tangu Mei 2016 na kujikutaka katika deni kubwa hilo.
Alisema uhakiki ulifanyika kwa kipindi cha kuanzia Mei 2016 hadi Februari mwaka huu , Kampuni ilikuwa inadaiwa jumla ya milioni 38.6 ikiwa ni michango ya watumishi na adhabu ya milioni 4,7.
Mussa alisema NSSF imejitahidi kumkumbusha mwekezaji huyo mara kwa mara kuwasilisha michango hiyo lakini amekuwa akikaidi kulipa na kutoa lugha zisizofaa na kumwomba Mkuu wa Mkoa kuingilia kati ili kampuni hiyo iweze kulipa stahiki za wafanyakazi wapatao 29.
Kwa upande wa Mhasibu wa kampuni hiyo, Musa Paschal amekiri kuwepo kwa deni hilo ambalo linatokana na malimbikizo ya michango ya muda mrefu ambayo haijawasilishwa NSSF.