Na Tiganya Vincent-RS-Tabora
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Aggrey Mwanri ameuagiza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge kushirikana na kampuni zenye leseni ya uchimbaji dhahabu kuhakikisha wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa eneo la Kitunda, wanapatiwa vitambulisho ikiwa ni njia ya kuimarisha usalama wakati wakifanya shughuli zao. Mhe. Mwanri alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza na Watendaji wa Halmashauri ya Sikonge na viongozi wa kampuni zote zilizopewa leseni ya uchimbaji madini ya dhahabu katika eneo la Kitunda. Alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuwatambua wachimbaji wadogo, wafanyabiashara na walioajiriwa ili kuepuka migongano ambayo imekuwa ukijitokeza kwa baadhi ya wachimbaji wadogo kuvamia machimbo ya wenzao wanaposikia yanatoa dhahabu na hivyo kusababisha mrundikano wa watu wengi katika shimo moja na kuhatarisha usalama wao. Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza kuwa vitambulisho hivyo pia vitasaidia kuwatambua wachimbaji wadogo wa kampuni moja na nyingine ili kuepuka vurugu. Alisema kuwa kabla ya zoezi hilo kufanyika ni vema uongozi wa Halmashauri na Kampuni zote uwe na taarifa sahihi za mhusika ikiwa ni pamoja na mahali alipozaliwa na uraia wake ili kuepuka kutoa ajira kwa wageni badala wachimbaji wadogo wadogo wa Kitanzania. Mkuu wa Mkoa ameagiza mtu yeyote kutoanza shughuli za uchimbaji mpaka atakapo sajiliwa katika daftari kubwa na lile na mitaa ili Serikali ijue ni nani waliopo hapo na wanatoka maeneo gani nchini.