Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RC Sendiga Akutana na Wazee wa Rukwa, Aomba Ushirikiano
Sep 12, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na. OMM Rukwa


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Queen Sendiga amewaomba wazee na viongozi wa madhehebu ya dini kuunga mkono jitihada za Serikali kusukuma agenda za maendeleo ili mkoa upige hatua za kiuchumi.

Sendiga amewasihi wazee hao kuliombea taifa na viongozi wake ili mipango inayowekwa izingatie maslahi mapana ya taifa na kujibu changamoto za maendeleo ya Rukwa hatua itakayowezesha ustawi wa jamii.

Mkuu huyo wa Mkoa ameyasema hayo leo (12.09.2022) mjini Sumbawanga wakati wa kikao na wazee pamoja na viongozi wa madhehebu ya dini toka katika wilaya zote tatu za mkoa wa Rukwa akiwa na lengo la kujitambulisha kwao na kuwaelezea mipango inayotekelezwa na Serikali.

“Nawaomba msaidie kuombea nchi yetu, tumwombee pia Rais wetu Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuiongoza nchi yetu vema katika kujiletea maendeleo kwani malengo yake ni mizuri”, alisema Sendiga.

Katika kikao hicho Sendiga aliwaeleza wazee kuwa wanalo jukumu la kusaidia na kushauri viongozi na watendaji wa Serikali ili shughuli za maendeleo za mkoa wa Rukwa ziwe kwa ubora hatua itakayoondoa changamoto kwa wananchi.

Nao wazee kwa nyakati tofauti akiwemo Honarama Mwimanza mkoani wa Sumbawanga alimkaribisha mkuu huyo kwenye mkoa wa Rukwa na kumsihi afuate nyendo za Rais Samia Suluhu Hassan katika kusimamia shughuli za maendeleo ya watu.

Kuhusu utekelezaji wa miradi , Meda Chipamba Mwenyekiti wa Wazee Kata ya Mazwi aliomba uongozi wa mkoa uwe na usimamizi wa karibu wa watendaji na wakandarasi wa miradi ili ikamilike kwani wananchi wengi wanakerwa na miradi mingi kutoisha.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Sendiga ametoa miezi miwili kwa Katibu Tawala Mkoa huo, Rashid Mchatta kukaa pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanamaliza tatizo la uwepo wa maboma ya shule yasiyokamilika na kupelekea watoto kukaa chini.

Sendiga ameyasema hayo leo wakati akizindua miongozo ya kuboresha elimu na kuongeza “Natamani kuona sekta ya elimu ikipiga hatua, usisikie raha kuona mkoa wetu uko nyuma kielimu” alisema Sendiga.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi