Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RC Mtaka: Simiyu Sasa Tunajadili Maendeleo ya Wananchi Siyo Mauaji ya Vikongwe na Albino
Oct 08, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Stella Kalinga, Simiyu

Mkoa wa Simiyu kwa sasa haujadili tena masuala ya mauaji ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) badala yake umejitikita katika kujadili na kushughulikia maendeleo ya wananchi wake. Hayo yamesemwa  jana na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Anthony Mtaka wakati akifunga Makambi ya Waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) yaliyoliyokuwa yakifanyika katika Uwanja wa Kidinda mjini Bariadi.

“Miaka hii miwili tumejenga mkoa ambao hatujadili tena mauaji ya albino, mauaji ya vikongwe wala watu kukatwa mapanga badala yake tunajadili Wasukuma, Wanyantuzu wanaokwenda kwenye maendeleo” alieleza Mtaka

Mkuu wa Mkoa huyo alibainisha kuwa kufuatia hali hiyo ndio maana hali ya makaazi ya mkoa imebadilika kwa kuongezeka ujenzi wa nyumba za gorofa na nyumba nyingine bora kwa kuwa wakaazi wa mkoa huo sio tena wale wanaoamini kuwa mtu “akiua anakuwa tajiri”.

Aliwataka waumini hao kuwa mabalozi katika kufanya mambo ya maendeleo  huku wakiwa mstari wa mbele kupinga na kukemea maovu katika jamii na kuwa mfano wa kuigwa katika kutenda mema.

Aidha, ametoa wito kwa waumini hao kuchangamkia fursa za miradi mbalimbali itakayotekelezwa mkoani humo ukiwemo mradi wa kilimo katika Skimu ya Umwagiliaji ya Mwasubuya Wilayani Bariadi, ambapo panakusudiwa kulimwa mpunga kupitia kilimo cha kisasa chenye tija.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa huyo amewataka waumini hao kuyafanyia kazi na kuyatafsiri kwa vitendo mafundisho waliyopewa wakati wa makambi yakiwemo ya ujasiriamali, ili mwaka kesho (2018) watu watakaoshiriki makambi kama hayo waone matokeo ya bidhaa zilizotengenezwa kutokana na ujuzi walioupata mwaka huu.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato na wananchi wote kwa ujumla kuwaombea viongozi wa Serikali hususan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kuwa anafanya kazi kubwa katika kudhibiti wizi na kutetea rasilimali za nchi ili ziwanufaishe Watanzania wote.

“Wapo watu wanauliza ni kwa nini Mhe. Rais aombewe, nawaomba tumuombee Mhe. Rais kwa sababu anafanya kazi kubwa kutetea rasilimali za Watanzania, anafanya maamuzi mazito ambayo yanawaumiza baadhi ya watu ambao wamekuwa wakijinufaisha wao na kuwaumiza wenzao;.......yanagusa biashara za watu ambao wakati mwingine wangetamani Serikali hii ife hata kesho, ni lazima tumuombee Mhe Rais” amesisisitiza Mhe. Mtaka.

Akimshukuru Mkuu wa Mkoa,  Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato wa Southern Nyanza Conference inayojumuisha Mikoa ya Simiyu, Mwanza, Shinyanga na Geita, Mchungaji Sadock Butoke  alisema, Makambi hayo yamekuwa ya mafanikio kwani pamoja na waumini hao kufundishwa Neno la Mungu, wamefundishwa masomo  ya afya, ujasiriamali, kaya na familia ambayo yatawaimarisha kimwili na kiroho.

Naye Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Simiyu, Mhe. Leah Komanya amewashukuru viongozi wa dini kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuisaidia Serikali kwa kuwaelekeza waumini wao kufanya mambo mema na kuwa na hofu ya Mungu, hali inayopelekea wananchi wengi kutojihusisha na vitendo viovu.

Makambi ya Waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato yamechukua takribani wiki tatu na yalifunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi