Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RC Malima Aridhishwa na Maendeleo ya MV Mwanza
Sep 02, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima amepongeza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza huku akiwasisitiza makandarasi  kukamilishaji mradi huo kwa wakati ili kuwanufaisha wananchi waishio kwenye ukanda wa maziwa makuu.


Hayo ameyasema leo tarehe 1.9.2022 baada ya kukagua mradi huo katika bandari ya Mwanza Kusini ambapo hadi meli hiyo itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kubeba magari madogo 20, magari makubwa matatu, tani 400 za mizigo na abiria 1,200 huku thamani ya mradi huo ikiwa ni Shilingi bilioni 96.9 na kutekelezwa na Kampuni ya Gas Entec ya nchini Korea.

 
"Nimefarijika sana leo kuwepo hapa, awali wakati mradi huu unaanza ilikua ni michoro tu kwenye makaratasi na ulikua ukisikia zile takwimu zinatajwa unadhani utani, Rais Mama Samia anatengezeza miundombinu kwa ajili ya wananchi wake na hiyo ndio dira ya Mhe. Rais wetu ya kuwatumikia wananchi wake na kwa kweli ameamua kuhakikisha mambo hayasimami, hivyo wananchi wa Mwanza wakae mkao wa kusafiri nayo." Alisema. 


Wakati akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Ndg. Eric Hamisi amesema kuwa meli hiyo inategemewa kushushwa  kwenye maji mwezi wa Oktoba kwa ajili ya matengenezo mengine yanayofanyika ndani ya meli ikiwemo kuweka viti na mifumo mengine. 


"Ujenzi wa hii Meli ulianza Januari, 2019 na ulikua uende kwa miaka miwili lakini zilitokea changamoto kadhaa ikiwemo ugonjwa wa Uviko 19 na mengineyo kutokana na hayo mkataba uliongezwa hadi mwezi Mei 2023 ambapo kwa sasa mradi umefikia asilimia 71 na hii ndio meli kubwa katika Ziwa hili na maziwa mengine nchini, hakuna meli kubwa kama hii kwenye ukanda wa maziwa makuu." Alisema.


Vilevile, ndg. Erick ameongeza kuwa ujenzi wa meli hiyo unafanywa na watanzania zaidi ya 200 wakishirikiana na wataalamu 6 kutoka nchini Korea.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi