Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RAS Tabora Aagiza Mzabuni Aliyeshinda Huduma Jazia Kuhakikisha Dawa Zipatikana Wakati Wote
Oct 30, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Tiganya Vincent - RS - Tabora

Serikali Mkoani Tabora imemtaka  mzabuni aliyeshinda na kusaini mkataba wa uanzishwaji wa Mfumo wa Mzabuni Mmoja kutoa huduma ya dawa na vifaa tiba (JAZIA- Prime Vendor System) kuhakikisha orodha ya dawa, vitendanishi vya maabara na vifaa tiba vilivyopo kwenye mkataba vinapatikana wakati wote ili kuepuka malalamiko kutoka kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Msalika Makungu wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba na Kampuni ya Chacha Magasi Pharmacy Ltd na Serengeti Care  kwa ajili ya kukabiliana na ukosefu wa dawa, vitendanishi vya maabara na vifaa tiba katika Vituo vyote vya Serikali mkoani humo ambazo hazipatikani Bohari Dawa (MSD).

Katibu Tawala Mkoa alisema afya bora ni kitu muhimu sana ndio maana Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetenga fedha nyingi kwa ajili ya dawa na vifaa tiba ili kuwawezesha wananchi kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo na kuongeza ndio maana hakuna sababu ya kutokuwepo dawa katika Kituo cha Afya chochote.

Aidha Makungu aliwataka Wakurugenzi Watendaji wote kuhakikisha wanasimamia makubaliano yaliyomo katika mkataba huo ikiwa ni pamoja na kuwahimiza wasimamizi wa vituo vya  kutolea huduma kuagiza dawa kutoka Bohari ya Dawa(MSD) na zile zitakazokosekana MSD ziagizwe kwa Mzabuni aliyeingia na Mkoa huo Mkataba na siyo vinginvyo.

Alisema ni vema wakawa wanafuatilia ili kuhakikisha Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali wakati wote zinakuwa na  dawa, vitendanishi vya maabara na vifaa tiba vya kutosha ili wagonjwa wasipate usumbufu.

Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Gunini Kamba alisema lengo la JAZIA ni kuboresha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba katika Vituo vya kutolea huduma, kuboresha uwazi na uwajibikaji kwenye matumizi fedha za umma na kupunguza muda wa kuomba na kupokea dawa na vifaa tiba.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi