Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Widodo Kuwasili Leo Nchini, Kufanya Ziara Siku Mbili
Aug 21, 2023
Rais Widodo Kuwasili Leo Nchini, Kufanya Ziara Siku Mbili
Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Mhe. Joko Widodo
Na Beatrice Sanga-MAELEZO

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kumpokea Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Mhe. Joko Widodo ikiwa ni ziara ya kiofisi ambayo imelenga kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa kidiplomasia wa nchi hizo.
 
Hayo yameelezwa Agosti 21, 2023 na Dkt. Stergomena Tax, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati wa mkutano na wahariri na waandishi wa habari ambapo alikuwa akielezea kuhusiana na ziara hiyo itakayofanyika nchini kuanzia Agosti 21 hadi 22, 2023.

Dkt. Stergomena amesema ziara hiyo ni matokeo ya kazi inayoifanywa na Rais wa Tanzania, Dkt. Samia ya kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na mataifa mengine ambayo imekuwa ni chachu ya viongozi mbalimbali duniani kutembelea nchini pamoja na shughuli mbalimbali za kimataifa kufanyika nchini.

“Mheshimiwa Rais Widodo atawasili tarehe 21 Agosti, 2023, na atapokewa rasmi na Mwenyeji wake, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 22 Agosti, 2023, Ikulu Jijini Dar es Salaam, baada ya mapokezi, viongozi hawa watakuwa na mazungumzo ya faragha, na baadaye mazungumzo rasmi, kabla ya hafla ya utiaji saini Hati za Makubaliano ya ushirikiano kwenye sekta mbalimbali kama afya, nishati, madini, uchumi wa buluu, ushirikiano wa kimataifa, uhamaji na biashara na kuzungumza na waandishi wa Habari,” amesema Dkt. Stergomena.

Dkt. Stergomena amesema kuwa, Rais Widodo atatembelea Ofisi ya Ubalozi wa Indonesia uliopo hapa nchini, huku akitarajiwa kushiriki dhifa ya chakula cha mchana iliyoandaliwa na Rais Samia kabla ya kuhitimisha ziara yake na kuondoka nchini.

Waziri Dkt. Stergomena amesema kuwa ziara hiyo inatarajiwa kuimairisha uhusiano uliopo kati ya nchi hizo mbili hususani katika maeneo ya kilimo na teknolojia kutokana na kwamba nchi hizo ni wanachama wa Umoja wa
Nchi zisizofungamana na Upande Wowote (NonAligned Movement–NAM) ambapo zimekuwa zikishirikiana katika masuala mbalimbali.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi