Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Mgeni Rasmi Kilele cha Mbio za Mwenge
Oct 11, 2024
Rais Samia Mgeni Rasmi Kilele cha Mbio za Mwenge
Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO, Bw. Thobias Makoba akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo Oktoba 10, 2024, jijini Dodoma kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa.
Na Lilian Lundo - MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wakati wa kilele cha mbio za mwenge na kumbukizi ya miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, zitakazofanyika mkoani Mwanza, Oktoba 14.

Hayo yameelezwa na Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO, Bw. Thobias Makoba, leo Oktoba 10, 2024, jijini Dodoma wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari alipokuwa akiongelea masuala mbalimbali ya kitaifa ikiwemo Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Kilele cha Mwenge wa Uhuru na Kumbukizi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

“Siku ya jumatatu tarehe 14 Oktoba, tukiwa tunakumbuka miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere tutafikia tamati ya zoezi la mwenge wa Uhuru na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Bw. Makoba.

Ameeendelea kusema kuwa, sherehe hizo zimetanguliwa na shughuli mbalimbali ikiwemo wiki ya vijana, ambapo Oktoba 11 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kasim Majaliwa Majaliwa anatarajiwa kufungua kongamano la vijana litakalojadili mada mbalimbali zenye maslahi mapana ya vijana wa nchi hii.

Aidha, baada ya kilele na shughuli za kuzima mwenge mkoani Mwanza, shamrashamra za mwenge wa uhuru zitaamia mlima Kilimanjaro, ambapo Mwenge wa Uhuru utawekwa juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro ilipoanzia historia ya mwenge huo.

Mwalimu Nyerere alisema, “....tunataka kuuwasha Mwenge na kuweka juu ya mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu; ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau", amenukuu Bw. Makoba.

Amesema kuwa, mwenge huo unapoenda kupanda Mlima Kilimanjaro utaleta upendo, amani, umoja na mshikamano kwa  Watanzania.

Mwenge wa Uhuru umefanyia kazi miradi 1,501 yenye thamani ya shilingi Trilioni 10. 8 katika halmashauri 180 kati ya 195 za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu unahusu Hifadhi ya Mazingira na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa chini ya Kauli Mbiu inayosema “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa endelevu”.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi