Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO, Bw. Thobias Makoba amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kesho Oktoba 11, 2024 anatarajia kujiandikisha katika daftari la mpiga kura katika Kijiji cha Chamwino, mkoani Dodoma ili atimize wajibu wake wa kupiga kura kama Mtanzania.
Bw. Makoba amesema hayo leo Oktoba 10, 2024, jijini Dodoma wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari alipokuwa akiongelea masuala mbalimbali ya kitaifa ikiwemo Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Kuanza kwa Bodi ya Ithibati, pamoja na Kilele cha Mwenge wa Uhuru na Kumbukizi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
“Katika kutimiza wajibu wa kidemokrasia, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Tanzania, siku ya kesho tarehe 11 Oktoba atajiandikisha katika kijiji cha Chamwino ili nae atimize wajibu wake wa kupiga kura kama Mtanzania. Basi, nasi wote tutimize wajibu wetu wa kujiandikisha ili tuweze kuchagua na kuchaguliwa kwa wale wataogombea nafasi mbalimbali,” amesema Bw. Makoba.
Amesema kuwa, ni rai ya Serikali kwa viongozi wote katika ngazi mbambali nchi kuwa mstari wa mbele kuwahamasisha Watanzania wenye sifa kujiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura katika maeneo yao.
Tarehe 27 Novemba, 2024 nchi yetu itakuwa na zoezi la uchaguzi wa tawala za mikoa na serikali za mitaa. Kulingana na ratiba ya uchaguzi iliyotolewa, kuanzia kesho tarehe 11 Oktoba mpaka tarehe 20 Oktoba kutafanyika zoezi la kuandikisha Watanzania wenye sifa kwenye orodha ya wapiga kura kwenye maeneo yao.
Zoezi la uandikishaji litafanyika katika vituo zaidi ya 80,812 vilivyopo nchi nzima, ambapo mwananchi atakuwa na sifa ya kupiga kura endapo atakuwa amejiandikisha katika daftari la uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Sifa za mpiga kura wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni kuwa Raia wa Tanzania, na umri wa miaka 18 au zaidi, kuwa mkazi wa eneo la kitongoji au mtaa husika na pia kuwa na akili timamu.
“Kupitia sifa hizi Watanzania wote wajitokeze kwa wingi katika vituo vilivyoandaliwa katika maeneo mnayoishi ili muweze kujiandikisha na kupata sifa na haki ya kupiga kura,” amesisitiza Bw. Makoba.