Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa kielelezo cha mafanikio makubwa yanayoendelea katika sekta ya michezo kwa kuhamasisha na kuweka mazingira mazuri ya michezo nchini.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha ameyasema hayo leo katika ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO kwenye program ya Idara hiyo inayoendelea ya Wakuu wa Taasisi kuzungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Taasisi za Serikali kwa miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Bi. Neema amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imeiongezea Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo bajeti kutoka shilingi bilioni 35.44 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi shilingi bilioni 258 mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo bajeti hiyo imeirahisishia wizara na taasisi zake kutekeleza majukumu yake.
"Katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Rais Samia, sekta ya michezo nchini imepiga hatua kubwa ikiwa ni ishara ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kukuza na kuendeleza michezo kama sehemu muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi", amesema Bi. Neema.
Ameongeza kuwa, Rais Samia ameleta mabadiliko ya kivitendo ambayo yameongeza ufadhili, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kisasa na ushirikiano wa kimataifa.
Katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya michezo, Rais Samia amefanya ukarabati mkubwa wa uwanja wa Benjamin Mkapa kwa takriban shilingi Bilioni 31, ameanza ujenzi wa uwanja wa michezo Arusha utakaogharimu shilingi Bilioni 338 na Dodoma kwa shilingi Bilioni 310. Pia, anajenga viwanja vya mazoezi kwa gharama ya shilingi Bilioni 24.
Ametaja mafanikio mengine kuwa ni ; Tanzania kuwa mwenyeji wa matukio makubwa ya michezo ya Kimataifa, kuondoa kodi kwa nyasi bandia, Tanzania kuwa Makao Makuu ya Sekretarieti ya Baraza la Michezo la Afrika Kanda ya Tano na kuanzishwa kwa Mfuko wa Michezo.