Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Awafunda Wahitimu Elimu ya Juu Zanzibar
Dec 28, 2023
Rais Samia Awafunda Wahitimu Elimu ya Juu Zanzibar
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wahitimu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) (hawapo pichani) mara baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA)
Na Ahmed Sagaff - Maelezo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wahitimu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kukabiliana vyema na changamoto za kimaisha zinazowakabili wahitimu wa elimu ya juu.

Akizungumza leo mara baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu ya Utalii na Usimamizi wa Masoko ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Rais Samia amemuomba Mwenyezi Mungu mtukufu awasaidie wahitimu hao.

"Mnakokwenda kuna changamoto nyingi sana za kimaisha, nendeni mkazikabili kwa njia chanya, na nataka niwaambie kwamba mkitoka hapa muwe na mawazo mema kwa sababu ukijiwazia mabaya, mpaka moyo wako utabeba mabaya, mdomo wako unabeba mabaya, na matendo yako yatakuwa mabaya, lakini ukiwaza mazuri basi kila kitu kinakwenda kuwa kizuri," Rais Samia amewaelekeza wahitimu hao.

Naye, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mkuu wa SUZA, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi ametaja idadi ya wanafunzi waliohitimu masomo yao ni 2,102 akisema ni ongezeko la asilimia tisa ikilinganishwa na idadi ya wahitimu 1,913 kwa mwaka wa masomo 2021/2022.

"Sina shaka kwamba wahitimu hawa 2,102 wameandaliwa vizuri sana, chuo chetu kitaendelea kuwa bora kwa kuandaa vijana kwa umahiri na wenye weledi kitaaluma wenye uzalendo na watakaotoa mchango muhimu katika sekta mbalimbali za maendeleo pamoja na kuhimili ushindani katika soko la ajira," Rais Mwinyi amewaeleza Watanzania.

SUZA ni taasisi ya  Elimu ya juu ambayo ilianzishwa mwaka 1999 na kuanza kutoa huduma zake rasmi mwaka 2001, kikwa ni miongoni mwa vyuo vikuu vilivyopo nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi