Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa Watanzania kwenda kujiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura wa Serikali za Mitaa kuanzia leo tarehe 11 hadi 20 Oktoba, 2024.
Mhe. Rais amesema hayo leo, Chamwino mkoani Dodoma wakati akizindua zoezi la uandikishaji wa Daftari la Wapiga Kura wa Serikali za Mitaa.
“Natoa rai kwa kila mmoja kwa nafasi yake kuanzia leo Oktoba 11 hadi Oktoba 20, 2024 kwenda kujiandikisha katika mitaa yao ili kupata nafasi ya kuchaguliwa au kuchagua kiongozi anayefaa kuwawakilisha,” amesema Mhe. Rais.
Amesema zoezi hilo la kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura wa Serikali za Mitaa lina umuhimu wake, kwani viongozi wanaochaguliwa wanasaidia katika suala la usalama na amani kupitia utambuzi wa watu kwenye maeneo wanayoyaongoza. Pia huduma nyingi zinawataka wananchi kuanzia kwa viongozi waliopo katika maeneo yao.
“Zoezi hili linaonesha uhuru wa demokrasia na tamaduni za nchi yetu, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka mfumo wa Tawala za Mikoa, hivyo usiposhiriki unakiuka katiba inayokuongoza ndani ya nchi yako,” amesema Mhe. Rais.
Aidha, amesema kuwa, mfumo huo ni wa kikatiba, hivyo kila mtu ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa, ambapo kwenye kuchaguliwa ni mtu yeyote mwenye sifa nzuri, kuanzia miaka 21.
“Naomba zoezi hili lifanywe kwa usalama na amani ili tusitie doa nchi yetu, tumalize chaguzi zetu za awali salama. Nawakumbusha kuwa zoezi hili ndio linalotoa taswira ya uchaguzi mkuu wa 2025, hivyo nawaomba tukachague vyema,” amesisitiza Mhe. Rais.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika siku ya Jumatano tarehe 27 Novemba, 2024, siku hii itatangazwa kuwa sio siku ya kazi ili wananchi wote wapate nafasi ya kup