Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa Watanzania na wadau wa sekta ya utalii kuona namna ya kuufanya utamaduni kuwa biashara ili ulete manufaa ya kiuchumi kwa nchi.
Ametoa rai hiyo wakati akihitimisha Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa lililofanyika wilayani Songea mkoani Ruvuma kuanzia Septemba 20 hadi 23, 2024 ambapo ametaja madhumuni ya matamasha ya utamaduni yanayofanyika nchini kuwa ni kuendeleza, kuenzi na kulinda tamaduni na mila za nchi pamoja na kufungua fursa za kiuchumi kwa Watanzania kupitia kazi za sanaa na utamaduni.
"Wakati naangalia mabanda ya maonesho, nilipita banda la BASATA na nimefurahishwa sana na mabadiliko ya sera ambayo BASATA wanafanya, wanabadilika na kuufanya utamaduni, sanaa na ubunifu kuwa ni ajira, biashara na uchumi. Huu ndio mwendo wa kwenda na nawatia moyo BASATA kusimamia vizuri hilo." Amesema Rais Dkt. Samia.
Amefafanua kuwa, kutokana na umuhimu wa utamaduni, Serikali imeamua kuyatumia matamasha hayo kudumisha utamaduni, mila na desturi na inafanya hivyo kwa sababu utamaduni wa Tanzania umefungamanishwa na misingi thabiti ya umoja, mshikamano, upendo, amani na utulivu viliyorithiwa kutoka kwa Waasisi wa Taifa hilo.
Akizungumzia lugha ya Kiswahili, amesema kuwa haiwezekani nchi ikaongelea utamaduni bila kugusia lugha hiyo kwani ndiyo inayowaunganisha Watanzania na kuwafanya kuwa na utamaduni mmoja, pia imefungua fursa za kiuchumi kwa Watanzania na kutokana na hilo, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imejipanga kufungua vituo vya lugha ya Kiswahili 100 kwa kushirikiana na Diaspora kote duniani.
Akieleza kuhusu suala la mmomonyoko wa maadili, ameitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na taasisi na wadau mbalimbali kulifanyia kazi suala hilo na kuja na mapendekezo ya namna bora ya kulishughulikia.
Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema katika kuuenzi na kuendeleza utamaduni wa nchi wametumia falsafa ya R4 ambayo Rais Samia ndiye mwanzilishi wake.
"Tamasha hili limefanya maridhiano kwa kushirikisha makabila yote ya Tanzania, tumetumia R4 kwa kutatua migogoro na changamoto za utamaduni, pia tumefanya mabadiliko ambapo sanaa hivi sasa ni ajira na inakuza uchumi." Amesema
Vile vile, amemshukuru Rais Samia kwa kukifanya Kiswahili kitambulike kimataifa ikiwemo katika Umoja wa Mataifa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).