Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Atoa Bilioni 9 Ufadhili Wataalam wa Afya
Aug 26, 2023
Rais Samia Atoa Bilioni 9 Ufadhili Wataalam wa Afya
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu mpango wa kila mwaka wa ufadhili wa masomo kwa Wataalam wa Afya katika kada mbalimbali ujulikanao kama "Samia Suluhu Super Specialists Program".
Na WAF - DSM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi  Bilioni 9 kwa ajili ya mafunzo ya wataalam wa fani za ubingwa  itayosaidia kukabiliana na changamoto ya upungufu wa fani hizo katika maeneo ya utoaji huduma za Afya kwa Wananchi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel Jijini Dar es Salaam wakati akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu mpango wa kila mwaka wa ufadhili wa masomo kwa Wataalam wa Afya katika kada mbalimbali ujulikanao kama "Samia Suluhu Super Specialists Program".

Amesema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ya Rais Samia ilitoa shilingi Bilioni 8 katika mpango huo na sasa imetoa shilingi Bilioni 9, ikiwa ni ongezeko la shilingi Bilioni 1.  

Dkt. Mollel amesema, mageuzi makubwa yanazidi kufanyika ndani ya Sekta ya Afya lengo ni kuhakikisha Wananchi wanapata huduma bora za matibabu ikiwemo yale ya kibingwa na ubingwa bobezi  hapa nchini.

“Kwenye eneo la ujenzi, tunashuhudia uboreshaji wa miundombinu, ajira za wataalam, ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, unaenda sambamba na kuendeleza taaluma za Wataalam wa Afya nchini ili waweze kutoa huduma bora za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi nchini,"

“Wizara ya Afya ilijiwekea lengo la miaka mitano (2020-2025) la kusomesha wataalam bingwa na bobezi wasiopungua 300 kwa kila mwaka wa fedha. Kupitia mpango huu wa ufadhili wa kuongeza wataalam bingwa na bozezi Tanzania (Samia Health Super Specialisation Program In Tanzania),” amesema Dkt. Mollel.

Aidha,  Dkt. Mollel  amesema Fedha hizi zitatumika kugharamia mafunzo kwa wataalam bingwa na bobezi 848 wanaoendelea na masomo katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi, huku akisisitiza Serikali  ya Dkt. Samia inatarajia kufadhili Wataalam wapya wasiopungua 300 kwa utaratibu wa kawaida pamoja na wataalam wengine wasiopungua 100 kwa utaratibu wa seti (Mfano seti ya; Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura, Muuguzi Bingwa, Daktari Bingwa wa ganzi na usingizi).

Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema, maombi yote yawasilishwe kwa njia ya kielektroniki kupitia tovuti https://esponsorship.moh.go.tz na kusisitiza kuwa maombi yatakayofanyiwa kazi ni yale yaliyowasilishwa kwa njia ya mfumo tu hivyo waombaji wanakumbushwa kufuata utaratibu uliowekwa.

“Ufadhili huu ni kwa ajili ya kulipiwa ada ya mafunzo, posho ya kujikimu na nauli kwa wanafunzi watakaopata ufadhili nje ya nchi. Pamoja na posho ya utafiti pindi mwanafunzi anapokuwa kwenye kipindi cha kufanya utafiti kama sehemu ya mafunzo yake,” amebainisha Dkt. Mollel.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi