Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Aonya Walafi Fedha za TASAF
Jun 01, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Ataka Viongozi wa Vyama vya Siasa wenye hali duni wasizuiwe kuingizwa kwenye mpango huo.

Na Grace Semfuko, MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya uhaulishaji wa kaya masikini zifanye kazi iliyokusudiwa ili kuliinua kundi hili kiuchumi.

Ameyasema hayo leo Juni 01, 2022 wakati akikabidhi magari mapya 123 yatakayotumika kwenye mpango huo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji zilizopo kwenye utekelezaji na kusisitiza kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya wanyonge na kwamba anazo taarifa za watu wanaotumia fedha hizo kwa matumizi yasiyokusudiwa.

"Mpango wa TASAF awamu hii kuna shilingi Trilioni 2, fedha hizi sio msaada ni mkopo nafuu, ili kuinua watu wetu walio chini sana kimaisha na kuwanyanyua, naomba mkatumie fedha hizi ipasavyo, nina taarifa kwamba kwenye baadhi ya maeneo bado kuna walafi, kuna watu wako midomo wazi, na wanafanya kila wanavyoweza wale fedha hii, na inapotokea kuna mmoja mgumu kula fedha hii huyo ndie anapigwa vita, fedha hii tunailipa watanzania wote kuweni na imani, chukua kile kinachopaswa, usichukue cha wanyonge, hii fedha ikafanye kazi iliyikusudiwa”, amesema Rais Samia.

Amewataka viongozi wa TASAF na Halmashauri kutoa elimu kwa wananchi wenye rasilimali ambazo zinaweza kuwapatia maisha mazuri lakini hawazitumii na kubakia kuwa na maisha duni huku akitolea mfano wafugaji wanaomiliki mifugo mingi lakini maisha yao yanaendelea kuwa duni, pia amewataka viongozi kuwatafutia masoko wanufaika wa mfuko huo ambao wanazalisha bidhaa huku akisisitiza wasaidiwe kuzipa thamani bidhaa hizo ikiwepo kutoa elimu ya uzalishaji pamoja na vifungashio.

Rais pia ametaka viongozi wa vyama vya siasa ambao wana hali duni ya maisha kuingizwa kwenye mpango huo wa TASAF ili kuinua uchumi wao.

"Tumesikia hapa kwamba uandikishaji na tahmini ya kaya unaendelea, sasa kwenye uandishikishaji wa kaya maskini ndugu Mwananga, kuna viongozi wa Vyama vya Siasa, ambao wamepewa vyeo vya vyama hivyo kule chini, hawa wameaminiwa na vyama vyao pamoja na wananchi wao, lakini ukimwangalia hali anaishi kwenye mazingira duni, kwa sababu kuwa na busara na hekima na kuaminiwa kwenye jamii hakuhitaji kuwa na pesa, unaweza kuwa na mazingira duni lakini ukaaminiwa kwenye jamii, kwa hiyo kama watu wamemchagua kuwa kiongozi wao kwenye eneo lile, na kama vigezo vyote anavyo kuwa anaishi kwenye mazingira duni basi isimzuie kufaidika na mpango huu wa TASAF.” Amesema Rais Samia.

Kuhusu magari aliyoyakabidhi wa Wakurugenzi, Rais ametaka yatumike kwa matumizi yaliyokusudiwa

"Magari haya yasiende kubeba magunia ya mikaa na kuni, magari haya yasiende kubeba abiria, madereva wakati wa jioni wanasombasomba, magari haya yakasimamiwe yasiende kufanya kazi hizo, na kwa upande mwingine hasa kule kwetu ninakotoka mimi, matumizi ya magari haya yanakwenda mashambani, hayatumiki kama yanavyopaswa, naomba sana viongozi wa TASAF mkasimamie rasilimali hizi, tutafuatilia mwenendo wa magari haya yatafungwa mfumo maalum wa Car trackinging, hii ni kuonesha yapo wapi na yanafanya nini”, amesema Rais Samia.

Kwa upande wake , Waziri wa Nchi,  Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema TASAF imeweza kutengeneza mifumo ya kuhuisha fedha na kuwafikia walengwa kwa wakati ambapo mfuko huo kwa kushirikiana na sekta na wizara nyingine imewezesha ujenzi wa miradi ya miundombinu ya kutoa huduma kwa wananchi katika sekta za Afya, Elimu, Kilimo, Miundombinu ya barabara na sekta nyinginezo

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF), Bw. Ladislaus Mwamanga amesema hivi sasa mfuko huo unatekeleza kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya mpango wa TASAF mpango ambao ulianza mwezi februari 2020 na kunatarajia kukamilika mwaka 2025 ambapo kipindi hiki kimetengewa Shilingi Trilioni 2.

Aidha, ameishukuru Serikali kwa kuidhinisha kuandikisha Kaya mpya 498,910 kwenye mpango wa TASAF ili ziweze kushiriki katika shughuli za kukuza uchumi wa kaya na pia kutoa fedha za UVIKO-19 shilingi Bilioni 5.5 ili ziweze kuwafikia walengwa wa TASAF katika maeneo yaliyo hatarishi kwa ugonjwa wa UVIKO- 19

TASAF ilianzishwa mwaka 2000 kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo katika jitihada za kupunguza umaskini kwa kutumia dhana ya ushirikishwaji jamii, program ya TASAF imetekelezwa kwa awamu tatu na imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali katika ngazi ya jamii kwa lengo la kupunguza umaskini kwa msingi wa kutoa huduma za jamii katika sekta zote, utekelezaji huo umekuwa ukizingatia mahitaji halisi au kero za wananchi wenyewe kwa kushirikiana na Serikali.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi