Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Aliagiza Baraza la Maadili Kusimamia Maadili Utumishi wa Umma
Apr 02, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Lilian Lundo - MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameliagiza Baraza la Maadili kusimamia maadili ya utumishi wa Umma  ili kila mtumishi wa Umma atambue majukumu yake na kuheshimu mipaka ya kazi yake.

Rais Samia amesema hayo leo, Aprili 2, 2022, Ikulu Chamwino Jijini Dodoma alipokuwa akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni wakiwemo Wajumbe wa Baraza la Maadili.

"Hali ya utumishi wa Umma sio nzuri sana, ingawa tunasifiwa kwa mabadiliko tuliyoyafanya Serikali ya Awamu ya Tano, yamekuza heshima kwenye Utumishi wa Umma, lakini heshima iliyokuzwa ni heshima ya uoga sio ya kutoka moyoni, sababu watu waliogopa kufokewa," alifafanua Rais Samia.

Aliendelea kusema kuwa, heshima inayotakiwa ni heshima ambayo inatoka moyoni,  na mtumishi awe na itikadi ya kujitambua kama ni Mtumishi wa Umma, na pia atambue majukumu yake ni yapi, nini anatakiwa kufanya na nini hatakiwi kufanya.

Aidha, amesema kuwa, kila mtumishi wa Umma ni lazima aheshimu mipaka yake ya kazi, bila kuingilia mipaka ya mtumishi mwenzake ili kuzuia migogoro ndani ya ofisi za Umma na kati ya kiongozi na kiongozi.

"Serikali inakwenda kuimarisha Chuo cha Utumishi pamoja na Chuo cha Uongozi ili kuweza kuwapatia mafunzo watumishi wa Umma. Baraza likisimama kwenye sheria na kurekebisha maadili ya watendakazi wa Tanzania tutakwenda vizuri," alisema Rais Samia.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewakaribisha viongozi hao ofisi ya Waziri Mkuu wakati wowote na kwa lolote ili kushirikiana na kutoa matokeo ambayo Mheshimiwa Rais anataka kuyaona kama ambavyo amekuwa akisisitiza wakati wote.

"Serikali na hasa Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia na shughuli za kila siku ndani ya Serikali tutawapa ushirikiano wa  hali ya juu ili mtekeleze majukumu yenu," alisema Waziri Mkuu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi