Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekagua na kupokea taarifa ya ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Songea ambao umekamilika kwa asilimia 100 Mkoani Ruvuma.
Rais Dkt. Samia amekagua kiwanja hicho, leo Septemba 23, 2024 mara baada ya kuwasili mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo, kuweka mawe ya msingi ya miradi na kuzungumza na wananchi.
Rais Dkt. Samia amepokea taarifa ya ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho uliohusisha upanuzi na kuongeza urefu wa barabara ya kuruka na kutua ndege, ujenzi wa maegesho mapya ya ndege (Apron), ujenzi wa barabara moja ya kiungio, ujenzi wa mnara wa waongoza ndege (Control Tower), kuimarisha maeneo ya usalama kiwanjani pamoja na ununuzi, usimikaji wa taa za kuongozea ndege na gari la zimamoto.
Akitoa taarifa mbele ya Rais, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 40.87 kukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho ambao hivi sasa utekelezaji wake umekamilika kwa asilimia 100.
Bashungwa ameeleza kuwa kukamilika kwa ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho umerahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kutoka ndani na nje ya nchi ambapo hivi sasa ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) zinatua mara 3 kwa wiki.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta ameeleza kuwa kazi zilizofanyika za uboreshaji wa kiwanja hicho ni pamoja na ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege (runway) kutoka mita 1,625 na upana wa 23 hadi kufikia mita 1,860 na upana wa mita 30 pamoja na ujenzi wa maegesho ya ndege (Apron) unaoruhusu ndege nne (4) aina ya Q400 Bombadier pamoja na ndege ndogo tatu (3) kupaki kwa wakati mmoja na hivyo kufanya kiwanja hicho kufikia kiwango cha 3C kwa mujibu wa viwango vya ICAO.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Abdul Mombokaleo ameeleza kuwa baada ya kukamilika kwa uboreshaji wa kiwanja hicho matarajio ni kuongezeka kwa idadi ya abiria ambapo takwimu zimeoneshwa toka mwaka 2021 abiria walikuwa 3,900 na sasa wamefikia abiria 19,620.
Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa kiwanja hicho ni utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.