Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Aing'arisha Geita
Oct 16, 2022
Na Jacquiline Mrisho


Na Lilian Lundo - Geita 


Meneja Miradi Tanesco, Mhandisi Didas Lyamuya amesema Serikali imetoa jumla ya Shilingi bilioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme cha Mpomvu kilichopo mkoani Geita chenye megawati 90. 


Mhandisi Lyamula amesema hayo leo katika mahojiano na Mwandishi wa habari hii, katika kituo hicho mkoani Geita. 


"Kituo hiki kimejengwa na Serikali ya Tanzania na kina uwezo wa kupoozesha umeme wa megawati 90, kimepokea umeme kutoka Bulyanhulu na kusambaza umeme katika Mkoa wa Geita na mikoa jirani," amefafanua Mhandisi Lyamuya. 


Ameendelea kusema kuwa, kabla ya kituo hicho kujengwa mkoa mzima wa Geita na Sengerema ulikuwa na jumla ya megawati nne tu, ambapo umeme huo ulikuwa unatokea Mkoa wa Mwanza, kilomita 1300. 


Mhandisi Lyamuya amesema kuwa, kituo hicho kinahudumia wateja 65,000 na pia kitu hicho kinauwezo wa kusambaza umeme katika maeneo ya migodi na viwanda. 


"Napenda kuwahakikishia kuwa tuna umeme wa kutosha na wa uhakika. Serikali ya Rais Samia imefanya kazi kubwa, kuhakikisha kituo hiki kinakamilika na kinafanya kazi inayokusudiwa," amefafanua Mhandisi Lyamuya. 


Kwa upande wake, mfanyabiashara wa mkoani Geita, Gofrey Shimiyu amempongeza Rais Samia kwa kuchapa kazi vizuri, kwani wanaona miradi mingi inatekelezwa katika mkoa wao wa Geita ukiwemo mradi wa kituo cha kupoozea umeme cha Mpovu. 


Naye, Afisa Habari wa Mkoa wa Geita,  Boaz Mazigo amesema Geita ilikuwa ina tatizo kubwa la umeme lakini kwa sasa tatizo hilo limeisha na umeme ambao unatumika ni kiasi kidogo sana cha umeme unazalishwa na kituo hicho cha Mpomvu, hivyo umeme mwingi unabaki bila matumizi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi