Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema suala la kukamilika kwa anwani za makazi na Postikodi nchini litakamilika kabla ya kufanyika kwa sensa ya watu na makazi mwaka huu.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akizungumza katika kilele cha maadhimisho Siku ya Sheria nchini.
“Hili litasaidia sana Muhimili wa Mahakama kwa kuwa hasa tunapotumia mahakama mtandao kwa sababu zile anwani za watu wanaokuja kuleta mashauri mahakamani lazima wajulikane wako wapi, hii ni sehemu muhimu kuelekea katika kufanyika kwa sensa ya watu na makazi”, amesema Rais Samia.
Aidha, amempongeza Jaji Mkuu, Prof. Ibrahim Juma, viongozi na watumishi wa Mahakama Kuu nchini kwa jitihada kubwa wanazofanya kwa kutumia teknolojia katika kutoa huduma za utoaji haki nchini.
“Mmeonyesha nia ya dhati na thabiti katika kuhakikisha kwa watanzania na wadau wote wa haki hasa wale wanaopata changamoto za kufikia huduma za haki mahakamani wanazipata kwa wakati na gharama nafuu, mmeweza kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kujenga na kufungua huduma kwenye maeneo yaliyokuwa hayana huduma na kujenga uwezo wa kutumia TEHAMA katika mawasiliano muhimu kwenye mnyororo wa utoaji haki hapa nchini”ameongeza.
Amesisitiza kuwa nchi haiwezi kubaki nje ya mapinduzi ya nne ya viwanda ambayo yanaendelea kubadilisha mizani ya ushindani katika shughuli zote za kibinadamu ikiwemo za uwekezaji na mazingira ya biashara na ili kufanikisha hilo ni lazima kuiboresha sekta ya sheria na utoaji haki nchini ili iweze kukabiliana na migogoro ya mashauri nchini na kutoa ufafanuzi wa kisheria katika mashauri hayo wakati wowote.
Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma amesema maboresho ya TEHAMA ambayo yamefanyika ambayo ni nyenzo muhimu katika utoaji haki imesaidia sana katika kuondoa changamoto.
Mahakama imejenga mtandao mpana wa TEHAMA ambao mahakama zote zimeunganishwa na imeongeza uwazi, uwajibikaji, taarifa zinapatikana kwa urahisi, maamuzi yanapatikana papo kwa papo bila kusubiri, zimeboresha shughuli za usimamizi, imepunguza gharama na muda wa mashauri.
Aidha, amesema kuwa safari ya mahakama mtandao haitafanikiwa kama itawaacha wananchi nyuma.
“Ni lazima tuwahusishe wananchi hasa katika kupata taarifa muhimu za kisheria”,amesema.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliezer Feleshi amesema Huduma ya mahakama mtandao inaendelea kufanya kazi za uendeshaji wa mashauri na kutoa haki kwa njia ya mtandao hivyo kuepusha ulazima wa wahusika kufika mahakamani.
“Kuanzia Januari mwaka huu hadi sasa, kati ya mashauri 5,447 yaliyofunguliwa mashauri 5,235 yalifunguliwa kielektroniki huku mashauri 212 pekee yalifunguliwa kwa njia ya kawaida”,amesema
Siku ya Sheria nchini huadhimishwa kila mwaka kuashiria kuanza kwa rasmi kwa shughuli za kimahakama kwa mwaka husika na mwaka huu ilikuwa na kauli mbiu inayosema Zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda: Safari ya Maboresho Kuelekea Mahakama Mtandao.