Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, ameyatahadharisha Mashirika ya Utangazaji ya Umma ya nchi za Kusini mwa Afrika kuhusu mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea duniani.
Akizungumza leo mjini Zanzibar, Mhe. Dkt. Mwinyi ameyataka mashirika hayo kutoachwa nyuma katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
"Tusipojipanga na kuwa tayari kwenda na mabadiliko, wakati utatulazimisha kubadilika, athari za kusubiri kubadilishwa na wakati zinaweza kuwa hasi na pengine kufanya mashirika ya utangazaji ya Umma kupoteza mvuto.
"Hivyo, napenda kutoa rai ya kuendelea kufanya uwekezaji katika mashirika yetu ya utangazaji kwa kuyawezesha kuwa na vitendea kazi vya kisasa vinavyoendana na maendeleo na mabadiliko ya sayansi na teknolojia duniani," amesema Rais Dkt. Mwinyi.
Naye, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Kundo Mathew amesisitiza umuhimu wa matumizi ya TEHAMA hususan katika kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya mapinduzi ya ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Ayub Rioba amesema Mashirika ya Utangazaji ya Umma yana umuhimu mkubwa kwa Waafrika katika zama hizi ambapo taarifa zinasambazwa sana kwa njia ya kidijitali.
Viongozi wa Mashirika ya Utangazaji ya Nchi za Kusini mwa Afrika wapo jijini Zanzibar wakijadili maendeleo ya mashirika hayo katika zama hizi ambapo matumizi ya TEHAMA yamekuwa ni nyenzo muhimu katika kuongeza tija na ufanisi.