Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Museveni Afanya Ziara ya Kikazi ya Siku 1 Hapa Nchini
Sep 13, 2020
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni leo tarehe 13 Septemba, 2020 amefanya ziara ya kikazi ya siku 1 hapa nchini ambapo ameungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kushuhudia utiaji saini wa makubaliano ya kukamilisha majadiliano ya utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Utiaji saini huo umefanyika katika uwanja wa ndege wa Chato Mkoani Geita ambapo Waheshimiwa Marais hao pia wametia saini waraka wa pamoja wa kuagiza kuanza haraka kwa utekelezaji wa mradi huo.

Hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Tanzania na Uganda wakiwemo Mawaziri, Wanasheria Wakuu wa Serikali, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi na wataalamu wa taasisi mbalimbali za Serikali na viongozi wa vyama vya siasa.

Waziri wa Nishati wa Tanzania Mhe, Dkt. Medard Kalemani amesema bomba litakalojengwa litakuwa na urefu wa kilometa 1,445 ambapo kilometa 1,149 kati yake zinapita nchini Tanzania, litapita katika mikoa 8, wilaya 24 na vijiji 280 hapa nchini, litakuwa na uwezo wa kupitisha mapipa 216,000 kwa siku, litazalisha ajira 10,000 na kwamba kwa miaka 25 ya mradi huo Tanzania itapata mapato ya kiasi cha shilingi Trilioni 7.5.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania Prof. Adelardus Kilangi amesoma maelekezo ya pamoja yaliyotolewa na kutiwa saini na Waheshimiwa Marais ambapo wameelekeza kuwa kila nchi ichukue hatua za haraka ili kutia saini mkataba kati ya nchi husika na kampuni zinazotekeleza mradi huo, kila nchi ianze kwa haraka mashauriano ili kusaini mikataba midogo inayohusika katika mradi huo na pia kila nchi ichukue hatua ili kuwezesha utekelezaji wa haraka wa mradi huo.

Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli amempongeza na kumshukuru Mhe. Rais Museveni kwa kuchukua hatua madhubuti za kutafuta mafuta nchini mwake, kukubali bomba lipitishwe nchini Tanzania na pia kuridhia asilimia 60 ya faida ichukuliwe na Tanzania (ambako bomba linapita kwa Zaidi ya asilimia 70) ilihali Uganda ikichukua faida kwa asilimia 40.

Mhe. Rais Magufuli amesema kutekelezwa kwa mradi huo ni ushindi mkubwa wa kiuchumi kwa Uganda na Tanzania pamoja na ukanda wote wa Afrika Mashariki na ameahidi kuwa Tanzania itasimamia masuala yote yaliyobaki ili utekelezaji uanze haraka kwa manufaa ya Watanzania na Waganda.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameeleza kuwa kutekelezwa kwa mradi huo kutarahisisha upelekaji wa gesi ya Tanzania nchini Uganda kupitia njia hiyo hiyo na pia kutarahisisha usafirishaji wa mafuta yanayotafutwa katika mbuga ya Wembele nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Mhe. Rais Museveni ameelezea kufurahishwa kwake na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo na amebainisha kuwa kwa sasa jambo muhimu ni kuanza utekelezaji wa mradi ili wananchi waanze kuona manufaa yake badala ya kupoteza muda mwingi zaidi katika majadiliano.

Mhe. Rais Museveni amesema utafiti uliofanywa katika asilimia 40 ya bonde la mto Albert huko Hoima nchini Uganda umebaini kuwepo kwa mapipa bilioni 6.5 ya mafuta ghafi na kwamba zipo dalili njema kuwa asilimia 60 za eneo ambalo halijatafitiwa pia kuna mafuta na kwamba Uganda inatarajia kupata mafuta mengine katika ukanda wa Kadamu.

Amesimulia kuwa baada ya kubaini kuwa wataalamu wa mataifa ya nje walikuwa wakimyumbisha katika mpango wake wa kupata mafuta nchini Uganda, aliamua kuchukua hatua za kuwasomesha vijana wa Uganda na baadaye vijana hao wakafanya utafiti na kisha kupata mafuta ambayo leo yamefikia hatua ya kuchimbwa, na pia ametoa wito kwa wananchi wa Tanzania na Uganda kuamka na kuchapa kazi za uzalishaji mali kwa maendeleo badala ya kuishia kuzalisha kwa kujikimu.

Mhe. Rais Museveni amerejea nchini Uganda.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Chato

13 Septemba, 2020.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi