Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Mnangagwa Akabidhi Dola Elfu Kumi kwa Chuo cha Wazazi Kaole.
Jun 29, 2018
Na Msemaji Mkuu

 

Na. Immaculate Makilika-  Bagamoyo

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnganagwa amekabidhi dola za kimarekani elfu 10, kwa Chuo cha Wazazi Kaole ikiwa ni mchango wake katika chuo hicho, ambacho aliwahi kupatiwa mafunzo ya ufundi wakati wa harakati za ukombozi za kusini mwa Afrika.

Akizungumza  wakati alipotembelea Chuo hicho leo mjini Bagamoyo, Rais Mnangagwa alisema kuwa amefurahia kuona chuo hicho kikiendelea ambapo hapo zamani mwaka 1963 walitumia kama kambi ya kijeshi  katika harakati za kupigania uhuru.

“Naishukuru serikali ya Tanzania na Msumbiji kwa kuendelea kutunza sehemu hii, pia na mimi ninapenda kuchangia kiasi cha fedha dola elfu 10 za kimarekani. Alisema Rais Mnangagwa”.

Rais Mnagangwa alisema kuwa amefurahi kufika chuoni hapo tena, ikiwa ni miaka 58 tangu amalize masomo katika chuo hicho ambacho kilikuwa kambi ya kijeshi kikiwa na takribani wakufunzi 58 kutoka nchi za Zimbabwe, Afrika kusini na Msumbiji.

Aidha, alisema amefarijika kuona kambi hiyo waliokuwa wakitumia wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika kuwa Chuo cha Mifugo na Kilimo.

Chuo cha Wazazi Kaole, kilichoanzishwa mwaka 1963 kilitumika kutoa mafunzo ya ufundi kwa wapigania uhuru wakati wa ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika, ambapo baadaye kilikabidhiwa kwa chama cha TANU kabla ya kuwa Chama cha Mapinduzi.

Rais Emmerson Mnangangwa aliwasili nchini Juni 28 kwa ziara ya siku mbili,ambapo alikubaliana na mwenyeji wake Rais Magufuli kuendeleza ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya Tanzania na Zimbabwe, pia wakuu hao wa nchi waliahidi kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji ili wafanyabiashara wa nchi hizo waweze kufaidika na fursa na rasilimali zilizopo kwenye nchi hizo.

Rais Mnangagwa amerejea Zimbabwe leo baada ya kumalizika kwa ziara yake ya siku mbili hapa nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi