Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli Ahutubia Siku ya Sheria
Feb 02, 2018
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wakati wa maadhimisho ya mwaka mpya wa mahakama ama Siku uya Sheria kwenye uwanja wa Mahakama kuu Ocean Road jijini Dar es salaam.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali inaunga mkono utekelezaji wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa Mahakama ili kuongeza ufanisi wa majukumu yake. Mhe. Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 01 Februari, 2018 wakati akihutubia katika siku ya sheria, maadhimisho ambayo yamefanyika katika Mtaa wa Chimala, Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam, yakiwa na kauli mbiu “Matumizi ya Tehama katika utoaji wa haki kwa wakati na kuzingatia maadili”. Pamoja na kuunga mkono matumizi ya TEHAMA kwa Mahakama, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Mahakama kwa kazi inayoifanya ikiwemo kupunguza mrundikano wa kesi na ameahidi kuwa Serikali ipo tayari kusikiliza ushauri wa Mahakama juu ya maslahi ya wafanyakazi utakaotolewa mwezi huu na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiongea jambo na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa  Ibrahim Juma baada ya kuhutubia katika maadhimisho ya mwaka mpya wa mahakama ama Siku uya Sheria kwenye uwanja wa Mahakama kuu Ocean Road jijini Dar es salaam.

Pia Mhe. Rais Magufuli amesema yupo tayari kufanya uteuzi wa Majaji wengine kadiri atakavyoshauriwa na Mahakama ili kukabiliana na changamoto ya upungufu mkubwa wa Majaji iliyosababisha ongezeko kubwa la mrundikano wa mashauri katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.

Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Mahakama kuendelea kurekebisha dosari ambazo zimekuwa zikiuchafua mhimili huo wa Dola ikiwemo Majaji na Mahakimu kujihusisha na vitendo vya upokeaji wa rushwa na ucheleweshaji wa kesi ambavyo vinasababisha hasara kubwa kwa Taifa.

“Nilikuuliza Mhe. Jaji Mkuu na mimi nasema kwa uwazi kabisa, katika vibali vingi vya kusafiri nje ya nchi ninavyoombwa na Majaji na ambavyo vyote huwa ninaruhusu, na vimenisaidia kufanya utafiti wangu, wengi huwa wanaomba kwenda likizo nje ya nchi, Afrika Kusini, Uingereza, nakadhalika, na wanaenda na familia zao, wanakaa huko kwa siku 28, na pale chini wanaandika kuwa watajigharamia, hili huwa ni swali ninalojiuliza sana, maana mshahara wa Jaji ninaujua.

“Na ukweli huwa nafuatilia anapokwenda kule anakaa hotel na nani amehusika kulipa hotel hiyo yenye gharama za juu, na kwa nini ni fulani fulani tu, Mhe. Jaji Mkuu majibu hujayapata na mimi sijayapata, sasa Mhe. Jaji Mkuu fuatilia hili” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Jaji Mkuu Profesa Ibrahim  Juma na Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Othman Omar Makungu, , Naibu spika Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Sheria na Katiba Profesa Palamagamba Kabudi na  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais  - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora -  Mhe George Mkuchika katika picha ya pamoja na Majaji  Wastaafu baada ya kuhutubia wakati wa maadhimisho ya mwaka mpya wa mahakama ama Siku uya Sheria kwenye uwanja wa Mahakama kuu Ocean Road jijini Dar es salaam.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Jaji Mkuu kwa hatua alizochukuwa kuwafukuza kazi watumishi 112 wa Mahakama wakiwemo Mahakimu 17 waliojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili na amevishangaa vyombo vingine ambavyo hushirikiana na Mahakama kama vile Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Magereza na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa kutowawajibisha watumishi wake wanaokiuka maadili. “Mwaka jana nililalamika, sasa mwaka huu sitalalamika, nitachukua hatua, tena mwezi huu wa pili hautaisha, pale ofisini kwangu napokea barua nyingi za malalamiko ya ucheleweshaji wa kesi, kila kesi upelelezi haujakamilika, ni lazima kuwe na utatuzi wa jambo hili, hivi sasa kuna kesi za Shilingi Bilioni 169.1 na Dola za Marekani Milioni 38.2 zinasubiri tu na nchi inakosa mapato” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli. Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli amemtaka Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi, kukamilisha kanuni za sheria ya msaada wa kisheria (Legal Aid Act, No.1 of 2017) ambayo imepitishwa na Bunge na kusainiwa na Rais tangu miezi 9 iliyopita, ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia sasa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Makamu wa Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Mhe. Godwin Ngwilimi  baada ya kuhutubia katika maadhimisho ya mwaka mpya wa mahakama ama Siku uya Sheria kwenye uwanja wa Mahakama kuu Ocean Road jijini Dar es salaam.

Mapema kabla ya hotuba ya Mhe. Rais Magufuli Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alisema Mahakama imedhamiria kuanza matumizi ya TEHAMA katika shughuli zake na ametaka watumishi hasa Majaji na Mahakimu wajiandae kutumia teknolojia hiyo, na pia ameahidi kuwa Mahakama itaendelea kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya ukiukwaji wa maadili na kusimamia uwajibikaji.

Nae Makamu wa Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Mhe. Godwin Simba Ngwilimi amesema TLS inaunga mkono dhamira ya kutumia TEHAMA katika shughuli za Mahakama na amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi wake unaoakisi nia na matarajio ya Watanzania.

Gerson Msigwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU Dar es Salaam 01 Februari, 2018

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi