Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli Aweka Jiwe la Msingi Upanuzi Uwanja wa Ndege Mtwara
Apr 02, 2019
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 02 Aprili, 2019 ameanza ziara ya kikazi ya siku 3 Mkoani Mtwara ambapo mara baada ya kuwasili ameweka jiwe la msingi katika upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mtwara na kuzungumza na wananchi.

Uwanja huo unafanyiwa upanuzi ikiwa ni miaka 67 tangu ulipojengwa mwaka 1952 ambapo upanuzi unahusisha kuongeza upana wa njia ya kurukia kutoka meta 30 hadi 45, kuongeza urefu wa njia ya kurukia kutoka meta 2,258 hadi 2,800, kujenga maegesho mapya ya ndege, kujenga barabara na maegesho ya magari, kuweka vifaa vya zimamoto na usalama, kujenga uzio na kuweka mfumo wa umeme wa akiba.

Upanuzi huo umeanza Juni 2018 na utakamilika Septemba 2020 kwa gharama ya shilingi Bilioni 50.4, fedha ambazo zimetolewa na Serikali ya Tanzania.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Christianus Ako amesema upanuzi huo ukikamilika utauwezesha uwanja wa ndege wa Mtwara kupokea ndege za daraja 4E ambapo ndege kubwa na ndogo zitakuwa na uwezo wa kutua na kuruka.

Akizungumza katika sherehe hizo Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano imemua kuupanua uwanja huo ili kufungua fursa nyingi zaidi za kiuchumi katika mkoa wa Mtwara na kwamba upanuzi kama huo unafanywa katika viwanja vingine 11 hapa nchini.

Kuhusu kuchelewa kuanza kwa kazi za upanuzi huo kutokana na Mkandarasi M/S Beijing Construction Engineering Group Company Ltd kutopatiwa sehemu ya malipo ya awali, Mhe. Rais Magufuli ametoa siku 5 kwa Mawaziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha asilimia 15 ya awali ambayo ni sawa na shilingi Bilioni 7 zinalipwa,lakini amemuonya Mkandarasi huyo kuhakikisha anafanya kazi vizuri (usiku na mchana) na kwa kuzingatia muda kwa kuwa taarifa zinaonesha Mkandarasi huyo hajafanya kazi ya kuridhisha katika uwanja wa ndege wa Mwanza.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amezungumzia ununuzi wa korosho uliofanywa na Serikali baada ya wanunuzi binafsi kutaka kununua korosho kwa bei ya chini ya shilingi 2,000 na kueleza kuwa baada ya Serikali kuamua kununua korosho hizo kwa shilingi 3,300 kwa kilo, jumla ya tani 156,865 zenye thamani ya shilingi Bilioni 578.7 kutoka kwa wakulima 373,149 zimenunuliwa na hivyo kuwaokoa wakulima hao wasipoteze mapato makubwa.

Kufuatia baadhi ya wenye korosho zinazozidi kilo 1,500 kukiri na kuomba radhi baada ya kushindwa kuuza korosho zao kwa Serikali kutokana na kuzikusanya kwa njia zisizokubalika (Kangomba), Mhe. Rais Magufuli amekubali kuwasamehe na ameagiza Wizara ya Fedha na Mipango kutoa shilingi Bilioni 50 katika siku 2 zijazo ili waanze kulipwa.

Hata hivyo ameonya kuwa watakaoruhusiwa kuuza ni wale wanaozimiliki korosho hizo dosari nyingine na ametaka mchezo wa kununua korosho kwa mtindo wa Kangomba ukome.

“Najua kuna watu 18,000 wakiwemo wale wasiokuwa na mashamba 780 hawajalipwa, nimeshatoa maagizo zitolewe shilingi Bilioni 50 ili waanze kulipwa, nafanya hivi kwa sababu wamekiri na wameomba radhi kwa kufanya kangomba, sasa msirudie tena mchezo huu, achene kuwanyonya wakulima” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Katika mkutano huo Mhe. Rais Magufuli amewaonya viongozi wa Mkoa wa Mtwara kuacha kugombana wao kwa wao na badala yake amewataka washirikiane kusukuma mbele gurudumu la maendeleo la mkoa huo. Pia amewaomba viongozi wa Dini wasaidie kuwaunganisha viongozi hao.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Mtwara

02 Aprili, 2019

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi