[caption id="attachment_35073" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, Mawaziri, Viongozi wa dini na Chama akivuta utepe kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa Daraja la Mto Sibiti lenye urefu wa mita 82 pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa km 25 katika eneo la mto Sibiti Mpakani mwa Simiyu na Singida.[/caption]
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la mto Sibiti litakalounganisha Mikoa ya Singida na Simiyu pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa jumla ya kilometa 25.
Daraja hilo lenye urefu wa meta 82 linajengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 20.172 na ujenzi wake unahusisha ujenzi wa nguzo kubwa 3 zenye kimo cha meta 7 kila moja, na pia linajengwa tuta lenye kimo cha meta 11 na makalvati 66.
[caption id="attachment_35074" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, Mawaziri, Viongozi wa dini na Chama akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mitambo itakayotumika katika mradi huo wa ujenzi wa Daraja la mto Sibiti.[/caption] Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi huo umefikia asilimia 80 na kwamba utakamilika ifikapo mwezi Machi, 2019.Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa na kasi ndogo ya ujenzi wa daraja hilo na ameitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na TANROADS kumsimamia mkandarasi kwa ukaribu ili ujenzi ukamilike haraka.
“Haiwezekani ujenzi wa daraja hili uchukue miaka 6 wakati wananchi hapa wanapata shida hasa wakati wa mvua, mkandarasi amelipwa fedha zote anazostahili nataka afanye kazi usiku na mchana, nataka nikirudi hapa nipite juu ya daraja, kama mkandarasi hawezi kumaliza kazi haraka mfukuzeni” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
[caption id="attachment_35075" align="aligncenter" width="750"] Wanachi mbalimbali kutoka Singida, Maswa, Sibiti wakishangilia wakati wa hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika eneo la Sibiti mpakani mwa mikoa ya Simiyu na Singida.[/caption] [caption id="attachment_35076" align="aligncenter" width="750"] Sehemu ya Daraja la mto Sibiti lenye urefu wa mita 82 upana mita 10.5 linalounganisha kati ya mikoa ya Simiyu na Singida kama linavyoonekana ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 70.[/caption]Kuhusu mvutano wa sehemu ambazo barabara itapita kuunganisha Mikoa ya Singida na Simiyu kupitia daraja la mto Sibiti, Mhe. Rais Magufuli amesema barabara ya kiwango cha lami itajengwa kati ya Chemchem – Sibiti – Meatu.
Mhe. Rais Magufuli pia amezungumzia pikipiki 2,800 zilizotolewa na Serikali kwa Waratibu Elimu Kata nchi nzima na kutaka pikipiki hizo zitumike vizuri kusaidia usimamizi wa elimu na kwamba wanaokabidhiwa pikipiki hizo wasaini mikataba ili wawajibike endapo wataziharibu au kuibiwa.
Mapema akitoa salamu za Mkoa wa Singida, Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Rehema Nchimbi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali kutoa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma za kijamii katika Mkoa huo, ikiwemo shilingi Bilioni 24 za elimu bila malipo, pikipiki 136 za Waratibu Elimu Kata, shilingi Bilioni 8 za kujengea vituo vya afya 10, kuongeza usambazaji wa umeme kupitia mradi wa umeme vijijini awamu ya 3 (REA III) na kujengwa kwa daraja la Sibiti.
Hafla ya uwekaji jiwe la msingi la daraja la mto Sibiti ambalo ujenzi wake unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, viongozi wa dini, viongozi wa Mikoa ya Singida na Simiyu, Wabunge na wananchi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Singida
10 Septemba, 2018