Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli Awataka Viongozi wa Dini Kuhubiri Upendo na Amani
Nov 05, 2018
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_37746" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Waumini mbalimbali wa Kanisa Katoliki, Maaskofu pamoja na Wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji, Afya na Elimu mara baada ya Misa iliyofanyika Bagamoyo Mkoani Pwani.[/caption]

Na. Immaculate Makilika

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wa dini kuhubiri amani, upendo na mshikamano kwa watanzania ili kusaidia Taifa kusonga mbele kimaendeleo.

Akizungumza leo Mjini Bagamoyo mkoani Pwani, katika   misa maalum ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 150 ya kanisa Katoliki nchini Tanzania, Rais Magufuli alisema kuwa ni muhimu kwa viongozi hao wa dini kuhubiri upendo na amani kwa watanzania wa dini na makabila yote.

“Nataka muhubirie watanzania kuhusu upendo, amani na mshikamano, kwa vile naamini kuwa itasaidia kuondokana na matendo maovu na kwa njia hiyo tutaweza kulipeleka Taifa mahali pazuri”, alisema Rais Magufuli

[caption id="attachment_37745" align="aligncenter" width="750"] Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akiwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamini Mkapa pamoja na Spika Mstaafu Anne Makinda wakiwa katika Misa takatifu ya ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji, Afya na Elimu Bagamoyo mkoani Pwani.[/caption]

Rais Magufuli alitolea mfano  matendo maovu yanayotakiwa kukemewa na viongozi wa dini na ambayo jamii inatakiwa kuyaepuka kuwa ni rushwa, wizi na vitendo vya ubakaji.

Aidha, Rais Magufuli amelipongeza kanisa Katoliki nchini Tanzania kwa kuweza kufikisha miaka150 ya uinjilisti na kwa kubeba jukumu kubwa la kuisaidia jamii katika kutoa huduma za elimu na afya.

“Kazi nyingine kubwa iliyofanywa na  kanisa Katoliki  katika kipindi cha miaka 150 ni kutoa huduma katika vituo 777 vya elimu, ikiwa shule za awali 228, shule za msingi 262, shule za sekondari 173 shule za ufundi 110 na vyuo vikuu 4, pamoja na vituo vya afya zaidi ya 100 vilivyopo nchini nzima”, alisema Rais Magufuli

Sambamba na hilo, Rais Magufuli alisema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu ya dini zote, ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zainazowakabili viongozi hao wa dini.

Aidha, Askofu wa Jimbo la Mpanda  na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Gervas John Nyaisonga, alimpongeza Rais Magufuli kwa kutimiza miaka mitatu tangu kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na kuongeza kuwa amedhihirisha kwa vitendo kuwa anapenda viwango, nidhamu katika kazi na ulipaji kodi kwa wananchi.

Kwa upande wake, Balozi wa Italia nchini Tanzania, Roberto Mengoni,  aliwashukuru viongozi wa Serikali na kanisa kwa kupata heshima ya kuwakilisha nchi yake katika maadhimisho hayo muhimu.

[caption id="attachment_37747" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Muadhama Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Nairobi John Kardinal Njue ambaye aliongoza Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji, Afya na Elimu Bagamoyo mkoani Pwani.[/caption]

Naye, Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania,  Dkt. Detlef Waechter, alisema kuwa kanisa Katoliki nchini Tanzania limeendelea kukua na Serikali ya Ujerumani itaendeleza urafiki na ushirikiano uliokuwepo kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuendelea kusaidia jamii katika masuala ya elimu na afya.

Mnamo mwezi Machi mwaka 1868 wamishionari waliingia Bagamoyo mkoani Pwani, kwa lengo la kueneza injili ya kanisa Katoliki ambapo baadaye injili hiyo ilienea katika nchi mbalimbali ikiwemo Uganda, Kenya na Malawi.

Sikukuu ya maadhimisho ya miaka 150 ya uinjilisti ya kanisa Katoliki imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kanisa kutoka ndani na nje ya nchi, viongozi wa wastaafu wa Serikali, watendaji wa Serikali, pamoja na maelfu ya  waumini wa kanisa Katoliki nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi